Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba akizungumza wakati akifunga Kikao Kazi cha siku moja cha Uhamasishaji Wahariri wa Habari Kuhusu Usimamizi wa Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Sura 219, kilichofanyika leo Mei 16,2024 chini ya Uratibu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Mkoani Iringa.
Mkurugenzi Mkuu wa TMDA Dkt. Adam Fimbo, akizungumza katika kikao kazi hicho, alipokuwa akitoa hutuba yake ya utangulizi mapema kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi kuzungumza.
Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma (TMDA) Gaudensia Simwanza akizungumza alipokuwa akiwakaribisha Wahariri wa Habari na wadau wengine katika kikao kazi hicho cha siku moja Mkoani Iringa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba (kushoto), akisalimiana na Mwenyekiti mstaafu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, mara baada ya kumaliza kufungua rasmi kikao kazi hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba (kushoto), akifurahia jambo na baadhi ya Wahariri wa Habari alipokuwa akiwaaga baada ya kufungua Kikao kazi hicho.
Na: Hughes Dugilo, IRINGA
Serikali imewataka wananchi na wadau wanaosambaza Dawa na Vifaa Tiba Kinyume cha sheria kuacha mara moja kwani haitamuonea huruma mtu yeyote atakaekamatwa na Bidhaa hizo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba wakati akifungua Kikao Kazi cha siku moja cha Uhamasishaji Wahariri wa Habari Kuhusu Usimamizi wa Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Sura 219, kilichofanyika leo Mei 16, 2024 Mkoani Iringa.
Serukamba amesema kuwa Dawa na Vifaa Tiba ni bidhaa nyeti na zenye madhara makubwa, na kwamba ikiwa havikudhibitiwa ipasavyo zinaweza kusababisha ulemavu na kupoteza maisha, hivyo kudhoofisha uchumi wa nchi.
“TMDA ina jukumu la msingi katika kuhakikisha afya ya wananchi inalindwa na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha bidhaa zilizopo katika soko ni salama na zenye ubora” amesema Serukamba.
Aidha, katika kukabiliana na changamoto hiyo, amewasihi Wahariri wa Habari kuendelea kushirikiana na TMDA kupitia matumizi ya kalamu na zao kutoa elimu kwa jamii kwani kwa kufanya hivyo jamii itaweza kuifahamu Taasisi hiyo na kazi zake hivyo kuweza kutoa taarifa pale wanapotilia mashaka ya ubora na usalama wa bidhaa za Dawa na Vifaa Tiba zilizopo sokoni ili hatua stahiki zichukuliwe.
Akizungumzia uwepo wa matangazo ya Dawa kichume cha sheria, amesema Mamla hiyo ina jukumu la kudhibiti matangazo ya bidhaa hiyo ili kuzuia matangazo yenye nia ya kupotosha umma kwa lengo la Kibiashara.
“Napenda kuwaeleza kuwa suala la kudhibiti matangazo ni la Kisheria na katika kutekeleza Utekelezaji wake, zipo Kanuni za Udhibiti Matangazo ya Dawa na Vifaa Tiba zilizoandaliwa chini ya Sheria Sura 219 zilizoanza kutumika mwaka 2010” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TMDA Dkt. Adam Fimbo, amesema pamoja na jitihada za Mamlaka hiyo katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu shughuli za Udhibiti wanazofanya, bado uelewa uko chini kitu kinachoathiri utendaji wa Mamlaka hiyo.
“Kiwango hiki cha uelewa kinasababisha matumizi yasiyo sahihi ya Dawa, idadi ndogo ya wananchi wanaoripoti maudhui ya Dawa na baadhi ya wafanyabiasha kuingiza Dawa duni na bandia, pamoja na wananchi kutozingatia tarehe ya kuisha matumizi ya bidhaa” amesema Dkt. Fimbo.
Aidha ameongeza kuwa hali hiyo inapelekea Mamlaka kuendelea kutumia mbinu mbalimbali kuelimiaha jamii.
“Mamlaka inatambua mchango wa vyombo vya Habari katika kuongeza ulewa wa wananchi kuhusu shughuli za Udhibiti zinazofanywa na Mamlaka na kwamba uelewa mzuri wa waandishi na Wahariri wa vyombo vya Habari ni msingi wa uelimishaji jamii” ameongeza Dkt. Fimbo.
Katika kikao kazi hicho mada saba zilitolewa ikiwemo Udhibiti wa bidhaa, Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Sura 219, Bidhaa bandia na Udhibiti wake na ufuatiliaji, pamoja na utoaji taarifa kwa madhara yatokanayo na Bidhaa.
Mada nyingine ni Huduma za Maabara ya TMDA, uzoefu wa Udhibiti katika Kanda ya kati, na mchango wa vyombo vya Habari katika Udhibiti.