Home LOCAL WAHARIRI TUMIENI MKUTANO WA MALEZI KUTOA ELIMU – WAZIRI DKT. GWAJIMA

WAHARIRI TUMIENI MKUTANO WA MALEZI KUTOA ELIMU – WAZIRI DKT. GWAJIMA

Na: WMJJWM, Dar Es Salaam

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewaasa Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini kushirikiana na Serikali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu dhana ya Mpango wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto yaani MMMAM kupitia vyombo vya Habari.

Akizungumza na baadhi ya Wahariri hao jijini Dar Es Salaam Februari 26, 2024 ikiwa ni kuelekea mkutano wa Kimataifa wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, Waziri Dkt. Gwajima amesema Tanzania imepata fursa ya kuandaa mkutano huo kutokana na kufanikiwa kwenye kuandaa na kutekeleza Program Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto yaani JPT – MMMAM ya 2021/2022- 2025/2026.

“Nawaomba mtumie vyombo vya habari kuwakaribisha viongozi na wataalam wa MMMAM kwenye vyombo vyenu ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu dhana ya MMMAM na uwepo wa mkutano huo hapa nchini, kuandaa maudhui kuhusu MMMAM ili yasambazwe kupitia kwenye vyombo vya habari mnavyosimamia kabla ya mkutano, wakati wa mkutano na baada ya mkutano ili dhana hii iwe endelevu” amesema Waziri Gwajima na kuongeza

Mkutano huo utakaofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 14 Machi 2024 unatarajiwa kufunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na utajumuisha washiriki zaidi ya 1,100, kati yao washiriki 700 wanatoka nje ya Tanzania ikijumuisha nchi za Afrika Mashariki, Afrika, Ulaya na Amerika na zaidi ya washiriki 400 watatoka nchini Tanzania.

Waziri Dkt. Gwajima amefafanua kuwa, Tanzania imefanikiwa kuimarisha usimamizi na uratibu kwa kuwaleta pamoja Wadau wote wa kisekta wa Malezi na Makuzi ya Watoto ili kushirikiana kwenye kumhudumia mtoto kwa nyanja za malezi na makuzi yake kadri zilivyoainishwa na sayansi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto.

Amebainisha kwamba huduma zilizoainishwa kwenye Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ni Afya bora kwa mtoto na mama, Lishe ya kutosha, Malezi yenye kuitikia hisia za Mtoto na Ulinzi na Usalama wa Mtoto tangu anapokuwa tumboni mwa mama yake, anapozaliwa hadi anapofikia umri wa miaka 8.

Aidha, amesema katika mkutano huo wa kitaaluma utahusisha mijadala ya kando, mikutano ya viongozi wa ngazi ya juu na mkutano maalumu na waandishi wa habari ukijumuisha Viongozi wa Nchi za Afrika na Wadau wa Maendeleo. Kutakuwa pia na uzinduzi wa Mkakati wa Uchechemuzi wa Program ya Taifa ya MMMAM na uzinduzi wa Kampeni ya kuelimisha Jamii kuhusu Malezi na Matunzo ya Mtoto. Kadhalika, kutakuwa na maonesho ya afua zinazotekelezwa na Wadau wa Malezi ya watoto kuhusu MMMAM.

Kuhusu Kaulimbiu ya Mkutano wa Kimataifa wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa mwaka 2024 Waziri Gwajima amesema ni; Wekeza katika Malezi na Makuzi ya Watoto Wadogo; Kujenga Rasilimali Watu yenye Tija inayohimiza wadau wote wakiwemo Watoa maamuzi, Watunga Sera, Viongozi wa Kijamii na Wazazi kuwekeza katika Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto.

Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Jukwaa la Wahariri Angella Akilimali ameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kuwashirikisha wadau wa Habari na kuahidi ushirikiano wao kuelekea mkutano huo.

“Sisi tukiwa Jukwaa la wahariri, tunaahidi kutekeleza masuala yaliyoainishwa katika kikao hiki. Tutaandaa vipindi, kuandika makala mbalimbali na tukiwa ni wazazi na walezi tumeona jambo hili limetusaidia kwenye kazi zetu” amesema Angella.

Akitoa salaam za azaki, zitakazo shiriki kwenye mkutano huo, Mkurugenzi wa Mtandao wa Malezi na Makuzi nchini Mwajuma Rwembagila amesema wadau wanaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha utekelezaji wa programu ya MMMAM inafanikiwa kwa ustawi wa watoto na Taifa kwa ujumla ambapo hadi sasa wameifikia Mikoa yote 26 na Halmashauri 120 huku wakiwa mbioni kukamilisha kwenye Halmashauri 24 zilizo salia kukamilisha jumla ya Halmashauri 184.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here