Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mgeni wake Rais wa Romania Mhe. Klaus Iohannis wakati wakishuhudia utiaji saini wa Mikataba mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi hizo iliyotiwa saini na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) Prof. Raphael T. Chibunda na Waziri wa nchi wa masuala ya Dunia na Mikakati ya Kidiplomasia wa Romania Mhe. Traian- Laurentiu Hristea kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 17 Novemba 2023.
Tanzania na Romania zimetia saini Hati mbili za makubaliano moja ikihusu kukuza ushirikiano wa kiuchumi kisayansi na kiufundi katika sekta ya kilimo na mazingira.
Vile vile kumetiwa saini hati ya makubaliano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Romania kwa ajili ya kushirikiana katika kukabiliana na maafa na misaada ya kimataifa ya kibinadamu.
Utiaji saini huo umeshuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Romania nchini, Mhe. Klaus Werner Iohannis ambaye yupo nchini kwa ziara ya Kitaifa.
Rais Samia, akizungumza na waandishi wa habari amesema Marais hao wawili wamezungumzaia fursa zilizopo katika sekta za afya na utengenezaji wa dawa, kubadilishana uzoefu katika sekta ya kilimo ikiwemo usindikaji wa mazao na kukabiliana na majanga.
Aidha Rais Samia amesema mataifa hayo mawili yamekubaliana kuongeza wigo wa ufadhili wa masomo hususan kwenye fani za udaktari na famasia ambapo Romania imekubali kutoa nafasi kumi za masomo kwa Watanzania.
Wakati huo huo, Tanzania nayo imetoa nafasi tano za ufadhili kwa vijana wa Romania kuja kusoma kwenye vyuo watakavyovichagua ikiwa ni fursa ya kuchangia jitihada za Serikali za kujengea uwezo, rasilimali watu na kuimarisha huduma katika sekta mbalimbali.
Akizungumzia mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi wa COP28, 2023 Rais Samia amesema Tanzania inatarajia kuweka nguvu suala la nishati na nishati safi ya kupikia, hivyo amemuomba Rais Iohannis kuiunga mkono Tanzania.
Rais Iohannis yupo nchini kwa ziara ya Kitaifa ya siku nne yenye lengo la kuimarisha uhusiano baina ya nchi yake na Tanzania uliodumu kwa miaka 62 na ikiwa ni ziara ya kwanza kwa Mkuu wa Nchi kutoka Jamhuri ya Romania kutembelea nchini.
Zuhura Yunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu