Home SPORTS DKT. BITEKO AMTAKA MSAJILI WA HAZINA KUTOA MAELEZO

DKT. BITEKO AMTAKA MSAJILI WA HAZINA KUTOA MAELEZO

 *Ni kutokana na ushiriki hafifu wa mashirika ya umma michezo ya SHIMMUTA

*Ataka Watumishi kuwa weledi, watatue matatizo

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amemtaka Msajili wa Hazina nchini kufikia Jumanne Asbuhi awasilishe maelezo ya kwa nini mashirika mengi ya Umma hayajashiriki Michezo ya SHIMMUTA yanayoendelea jijini Dodoma, huku ikitambulika kuwa, mashindano hayo yalianzishwa na Serikali huku mlezi wake akiwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma wakati akifungua Mashindano ya SHIMMUTA yanayohusisha Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi ambapo awali, Mwenyekiti wa Kamati ya SHIMMUTA, Roselyne Massama alimweleza Naibu Waziri Mkuu kuwa wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya muitikio mdogo wa Mashirika ya Umma kushiriki mashindano hayo jambo ambalo linazorotesha mashindano hayo.

“‘Viongozi Serikali kama tumekubaliana kufanya jambo fulani basi tulifanye, na kama tunaona halifai basi bora tuliache, kuliko tunakubaliana kufanya kitu halafu hatukifanyi; haiwezekani viongozi wote hapa wanalalamika, Katibu Mkuu analalamika, Naibu Waziri analalamika na mimi nilalamike?, hapana sijaumbwa hivyo, sioni sababu yoyote ya kutamkika au ya kuandikika, kwamba kuna mashiriki ya umma 248 na hapa yapo mashirika 57 tu; haiwezekani.” Amesisitiza Dkt.Biteko

Aidha, amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, kuwaandikia barua Makatibu Wakuu wa Wizara ambao Taasisi zao hazijashiriki michezo hiyo, watoe maelezo kwanini hawajapeleka wafanyakazi kwenye mashindano hayo na yeye atashauri viongozi Wakuu wa Nchi, hatua za kuchukua.Vilevile, ameelekeza mashirika yote ya Umma yanayotakiwa kujiunga na SHIMMUTA kufanya hivyo.

Dkt.Biteko ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuiongoza na kuisimamia vyema Sekta ya Michezo na kuipa msukumo mkubwa ambao umefanya Taifa kutambulika zaidi duniani kote akitolea mfano kuchaguliwa kwa Tanzania kuwa moja ya nchi wenyeji wa michezo ya AFCON mwaka 2027.

Katika hatua nyingine, Dkt.Biteko ametaka Wafanyakazi nchini kufanya kazi kwa weledi na kuwahudumia Watanzania ipasavyo kwani Rais, Dkt.Samia anapima Watumishi kwa kazi zao, anataka kuwe na matokeo katika kazi hizo na ndio kipimo pia cha uwezo wa kuwahudumia Watanzania, hivyo lazima wasimamiane, wasibembelezane na wafanye kazi kwa taratibu zilizopo.

Pia amewataka Watumishi kuweka alama kwa kutoa huduma bora kwa wananchi, watatue matatizo ya wananchi na Taasisi zao zisiwe kikwazo cha Maendeleo.

Kuhusu ufadhili wa mashindano ya SHIMMUTA NA SHIMIWI, Dkt.Biteko ameitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kusimamia suala hilo ili michezo hiyo ifanyike kwa ufanisi.

Viongozi mbalimbali waliohudhuria Hafla ya Ufunguzi huo ni Mhe. Hamisi Mwinjuma, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Rosemary Senyamule, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Roselyne Massam Mwenyekiti wa SHIMMUTA.

Michezo hiyo ambayo mwaka huu imefikisha miaka 53 kutoka kuanzishwa kwake na Baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere, imejumuisha Taasisi 57 na wanamichezo walioshiriki ni 3478 huku michezo inayoshindaniwa ikiwa ni 12.

Kauli mbiu ya Maonesho hayo Michezo ni Afya na Uchumi: Tuwekeze kwenye Miundombinu ya Michezo kwa Afya Bora na Uchumi Himilivu! Kazi Iendelee.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here