Home BUSINESS WATUMISHI BRELA WAPATIWA ELIMU KUHUSU NHIF, WCF, UTT, WATUMISHI HOUSING, VYAMA VYA...

WATUMISHI BRELA WAPATIWA ELIMU KUHUSU NHIF, WCF, UTT, WATUMISHI HOUSING, VYAMA VYA USHIRIKA

     Bi. Ridhia Makono akitoa elimu kuhusu huduma zinazotolewa na Mfuko wa Bima ya Afya nchini (NHIF)

Bw. Pascal Masawe akisisitiza umuhimu wa kuwekeza kupitia fursa mbalimbali zinazotolewa na Watumishi Housing Investments

Baadhi ya watumishi wa BRELA wakifuatilia mafunzo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) , Mfuko wa Uwekezaji (UTT) na Watumishi Housing Investments Jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya watumishi wa BRELA wakiuliza maswali wakati wa mafunzo hayo

DAR ES SALAAM.

Watumishi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), wamepatiwa elimu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) , Mfuko wa Uwekezaji (UTT) na Watumishi Housing Investments ili waweze kuelewa na kutumia huduma na fursa zinazotolewa na Taasisi hizo ipasavyo.

Akifungua mafunzo hayo tarehe 9 Septemba, 2023 katika ukumbi wa Chuo cha Utalii, Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma na Uwezeshaji wa BRELA, Bw. Daimon Kisyombe amesema Mafunzo hayo kwa watumishi wa BRELA yamelenga kuwapa uelewa kuhusu huduma muhimu za afya zinazotolewa kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na taratibu za kuzingatia ili kupata huduma hizo na kuwapa elimu kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji zinazotolewa na Taasisi za Umma ili kuwajengea watumishi utamaduni wa kuwekeza kama sehemu ya kujiandaa na maisha baada ya kustaafu.

Pamoja na mafunzo hayo, watumishi walipata fursa ya kupewa elimu ya Ushirika ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuanzisha Chama cha Akiba na Mikopo kwa watumishi wa BRELA ili kupanua wigo kwa watumishi kupata fedha za kuwasaidia katika kujenga maisha yao ya sasa na baadaye.

Kupitia mafunzo hayo, watumishi walipata fursa ya kupitia na kuidhinisha Katiba ya Chama na kuteua uongozi na kamati muhimu kwa ajili ya kukamilisha taratibu za usajili wa Chama.

Akiwasilisha mada kuhusu huduma za NHIF Afisa Kutoka Taasisi hiyo Bi. Ridhia Makono anasema mfuko huo umekuwa ukihakikisha kuwa mwanachama anahudumiwa kulingana na michango inayotolewa na mwajiri kwa ajili ya matatibabu.

Amewataka watumishi kuzingatia miongozo inayotolewa na mwajiri kuhusu matumizi ya huduma za ziada zinazogharamiwa na mwajiri na kuepuka gharama zisizo za lazima zinazotokana na mambo yasiyohusiana na matibabu (lifestyle issues).

Kwa upande wake Afisa Mwandamizi kutoka Watumishi Housing Bw. Pascal Masawe amesema mtumishi anataiwa kuwekeza kuanzia sasa kwa kununua nyumba na viwanja kwa bei nafuu na kulipa kidogodogo mpaka hapo atakapokamilisha malipo na kuwa mmiliki wa halali wa nyumba au kiwanja.

Aidha Bw. Masawe amewahamisha watumishi kuchangamkia fursa ya kuwekeza katika mfuko wa Faida Fund kwa kununua vipande ambavyo thamani yake imekuwa ikiongezeka kwa haraka kwani katika kipindi cha miezi 9 thamani ya kipande imeongezeka kutoka TZS 100 kipindi cha Januari, 2023 hadi kufikia TZS 106.9 kipindi cha Septemba, 2023.

Naye Afisa Mwandamizi kutoka UTT AMIS Bw. Rahim Mwanga ametoa wasilisho kuhusu umuhimu na faida za kuwekeza katika mifuko iliyoanzishwa na UTT AMIS

Pia amefafanua kuhusu viwango vya uwekezaji na aina ya mifuko ambayo ni Umoja, Mfuko wa watoto, Mfuko wa Kujikimu, pamoja na Mfuko wa Ukwasi na kuwashauri Watumishi kujiunga na mifuko hiyo ili kuwa washirika katika uwekezaji ambao utaleta tija katika maisha yao.

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo yanayotolewa na BRELA kwa watumishi wake ili kuwajengea uelewa wa pamoja kuhusu masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na umuhimu wa kuzingatia Sheria na kanuni za utumishi wa umma ili kufanya kazi kwa ufanisi na kuchangamkia fursa mbalimbali za uwekezaji zinazotolewa na taasisi nyingine za Serikali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here