Home BUSINESS WATU ZAIDI YA 4,000 KUSHIRIKI MKUTANO WA MIFUMO YA CHAKULA JIJINI DAR

WATU ZAIDI YA 4,000 KUSHIRIKI MKUTANO WA MIFUMO YA CHAKULA JIJINI DAR

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akizungumza katika mkutano wa Wahariri na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu Septemba 3, 2023 Jijini Dar es Salam.

DAR ES SALAAM.

Zaidi ya washiriki 4,000 kutoka sehemu mbalimbali Duniani wanatarajiwa kushiriki Mkutano utakaojadili Mifumo ya Chakula barani Afrika ambao utafanyika Septemba 5-8, Dar es Salaam.

Chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, mkutano huo wa 13 utatoa fursa kwa viongozi, wataalam, wabunifu na wadau mbalimbali kujadili masuala tofauti yanayohusu sera, changamoto, mafanikio na ubunifu utakaoboresha sekta ya kilimo na mifumo ya chakula. Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu ya Dar es Salaam Septemba 3, 2023, Waziri wa Kilimo Tanzania, Hussein Mohamed Bashe, aliwakaribisha wageni kutoka ndani na nje ya nchi, kuhudhuria mkutano huo wa siku nne. Alisema mkutano huo ni hatua muhimu katika kuhakikisha bara zima la Afrika linakuwa na mifumo ya chakula endelevu na jumuishi.

“Mkutano wa mwaka huu unahimiza uwezeshaji wa wanawake na vijana, pamoja na kutambua umuhimu wao katika uzalishaji chakula barani Afrika,” alisema. Waziri Bashe.

pia, aligusia jinsi Serikali ya Tanzania inavyochukua hatua kuhakikisha upatikanaji wa chakula na kutengeneza ajira kupitia mpango wake wa BBT-YIA “Building a Better Tomorrow: Youth Initiative for Agribusiness (BBT-YIA)” ambao unalenga kutoa mafunzo kwa vijana 200,000 na kusaidia biashara za kilimo zipatazo 15,000 zinazofanywa na vijana, katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Mkutano huu utajadili namna ya kuongeza ajira za vijana kwenye mifumo ya chakula Afrika na kuonyesha biashara za kibunifu kwenye kilimo ambazo zinasimamiwa na wajasiriamali vijana.

Mkurugenzi mtendaji wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF)ambalo limeandaa mkutano huo, Amath Pathe Sene, alisisitiza umuhimu wa kushughulikia changamoto za mifumo ya chakula.

“Ni muhimu sauti zetu zisikike, tutoe masuluhisho yanayozingatia mazingira yetu na tutoe kipau mbele katika kuwawezesha wanawake na vijana katika mchakato wa kuboresha mifumo ya chakula,” alisema.

Mkutano huo pia unaandaa mjadala wa mifumo ya chakula kuelekea mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi (COP 28), utakaofanyika Dubai.

Mambo muhimu yatakayojiri katika mkutano huo ni pamoja na majadiliano ya wataalam, mkutano wa mawaziri zaidi ya 40, mkutano wa Wakuu wa Nchi ambao watatoa matamko yao kuhusu kuboresha mifumo ya chakula Afrika. Kwa taarifa zaidi kuhusu mkutano, ratiba na wazungumzaji, tembelea tovuti yetu https://agrf.org/summit/2023/

Kuhusu AGRF Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (Africa Food Systems Forum) ni jukwaa kubwa Duniani linalowaleta wadau pamoja kujadili hatua za kuboresha kilimo na mifumo ya chakula Africa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here