Mkazi wa Kata ya Nala katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma akiwa mwenye furaha akionesha kidole chake cha shahada kilichotiwa wino baada ya kupiga kura kuchagua Diwani wa Kata hiyo katika Uchaguzi mgogo unaofanyika Leo Septemba 19,2023 katika Kata hiyo. Aidha wananchi wa Jimbo la Mbarali na Kata zingine sita wanapiga kura kuchagua viongozi wao.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa Jacobs Mwambegele leo tarehe 19 Septemba, 2023 ametembelea na kukagua zoezi la kupiga kura kwenye Jimbo la Mbarali lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.
Jaji Mwambegele baada ya kutembelea vituo amesema ameridhishwa na utendaji wa Wasimamizi wa Uchaguzi huo na kuongeza kwamba vituo vimefunguliwa kwa wakati na zoezi linaendelea vizuri kwa utulivu na amani.
Aidha, Jaji Mwambegele amezungumza na mawakala wa vyama vya siasa ambao wamemueleza kuridhishwa na mwenendo wa zoezi la kupiga kura na kwamba hakuna changamoto yoyote iliyojitokeza.Â
Uchaguzi wa Jimbo la Mbarali unafanyika sambamba na kata sita za Tanzania Bara. Kata zenye uchaguzi ni Nala iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mfaranyaki iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Old Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo na Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.
Zoezi la kupiga kura likiendelea Kwa amani na utulivu katika vituo mbalimbali katika Kata ya Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Leo tarehe 19 Septemba, 2023
Wapiga kura wakiendelea kujitokeza kwenye vituo vya kupiga kura kwenye maeneo mbalimbali ya Kata ya Old Moshi Magharibi kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata hiyo iliyopo Halmashauri ya Moshi mkoani Kilimanjaro unaofanyika leo tarehe 19 Septemba, 2023.
Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mh.Jaji Asina Omari akitembelea na kukagua upigaji kura katika Kata ya Marangu Kitowo katika Halmashauri ya Rombo.