RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Serikali ya China kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa Tanzania ikiwemo Zanzibar kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo.
Dk. Mwinyi ametoa shukurani hizo Ikulu, Zanzibar alipowakabidhi vyeti na medali timu ya madaktari 32 kutoka China waliohudumu kwenye hospitali za Zanzibar kwa kipindi cha mwaka mmoja na kuwaaga baada ya kumaliza muda wao nchini.
Rais Dk. Mwinyi amesema, Zanzibar imenufaika na fursa nyingi kutoka China kupitia sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo Afya hususan kupokea timu za madaktari bingwa wanaofika nchini kubadilishana uzoefu na wazawa hali aliyoieleza imeimarisha uhusiano mwema uliopo baina yao pamoja na kujifunza uzoefu wa masuala mbalimbali ya afya.
Dk. Mwinyi alieleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendeleza maeneo mengi ya afya kwa kujenga hospitali zenye vifaa tiba vya kisasa, kuboresha miundombinu na kuongeza hospitali za wilaya na mikoa pamoja na kuifanyia matenegezo makubwa hospitali ya Mnazi Mmoja.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameshukuru kazi kubwa iliyofanywa na timu hiyo ya madaktari 32 kipindi chote walichohudumu Zanzibar na kusema Serikali ilnajivunia kuwepo kwao.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui ametoa Shukraani zake kwa timu ya madaktari hao nakueleza ushirikiano uliopo baina ya China na Zanzibar umedumu kwa miaka 60 sasa.
Naye, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk. Amour Suleiman Mohammed alisema timu hiyo ya madaktari bingwa kutoka China iliwasili nchini Septemba 26 mwaka 2022 na Septemba 26 mwaka huu inatarajiwa kurejea kwao.
Alisema timu hiyo ilitoa msaada wa kitabibu kwa wananchi wa Unguja na Pemba kwa magonjwa ya macho, meno, mkojo, figo, huduma za X- ray, pia ilifanya upasuaji kwa wagonjwa zaidi ya 50 kwa maradhi tofauti.
Kiongozi mkuu wa timu ya madaktari hao 32 , Dk. Zhao Xiaojun alishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano ilioutoa kipindi chote na kueleza Zanzibar ni visiwa vyenye upendo, amani na mshikamano kwa wenyeji na wageni.
“Kamwe hatutasahau uzuri na haiba ya mandhari ya visiwa vya Zanzibar vilivyopambwa kwa maumbile ya anga la buluu, fukwe nyeupe, uzuri wa mwanga wajua linapochomoza, kijani cha minazi na ukarimu wa watu wake, yote haya tutayakosa baada ya kuondoka Zanzibar” kwa hisia alisema.
Hata hivyo, timu ya madaktari hao ilimuahidi Dk. Mwinyi kuendeleza ushirikiano uliopo baina yao.