Na: Jacquiline Mrisho- MAELEZO
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ametoa rai kwa watumishi hasa wa mkoani Dodoma kuiga mfano wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) wa kuhamasisha watumishi wake kupanda miti katika maeneo mbalimbali ili kuendelea kutunza mazingira.
Mhe. Senyamule ameyasema hayo leo mkoani Dodoma wakati akifunga semina ya wastaafu watarajiwa wa Mfuko huo iliyofanyika kwa siku mbili kuanzia Septemba 25 – 26, 2023 mkoani humo.
Mhe. Senyamule ameipongeza PSSSF kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo mpaka sasa PSSSF imegawa miche ya miti kwa wastaafu watarajiwa na waliostaafu sasa wanafikia 739,000,
“Nimefurahi kusikia kuwa mmewashirikisha watumishi wa PSSSF kwa kuhakikisha kila mtumishi anapanda na kuitunza miche kumi ya miti, kampeni ambayo mmepanga iendelee hadi Disemba 2023 ambako mnatarajia mtakuwa mmepanda miche takribani milioni 7. Mimi na wenzangu mkoani, tunalipokea jambo hili jema kwa mikono miwili na natoa rai kwa watumishi wengine kuiga mfano huu”. Amesema Mhe. Senyamule.
Awali Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bi. Beatrice Musa – Lupi amesema kuwa Mfuko huo unatambua na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo umetoa mche mmoja wa mti kwa kila mstaafu mtarajiwa wa PSSSF aliyehudhuria semina wanazozitoa lengo likiwa ni kila mmoja aweze kuupanda na kuutunza mche aliopatiwa.
“Pia kwa kushirikiana na watumishi wa PSSSF tutaendesha kampeni ya kuhakikisha kila mtumishi anapanda na kuitunza miche kumi ya miti, kampeni hii itaendelea hadi Disemba 2023 ambapo tunatarajia kuwa tumepanda miche takribani milioni moja katika maeneo mbalimbali”, amesema bi. Beatrice.
Kwa upande wake Mstaafu mtarajiwa, Mhandisi Salum Omary ameishukuru PSSSF kwa kugawa miti kwa wastaafu watarajiwa ili nao waendelee kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutunza mazingira. Aidha, ametoa rai kwa wastaafu watarajiwa wenzie kuendelea kupanda miti zaidi ya hiyo waliyopewa na PSSSF.