Home BUSINESS RC CHALAMILA: MKUTANO WA AGRF KULETA FURSA KWA WANANCHI

RC CHALAMILA: MKUTANO WA AGRF KULETA FURSA KWA WANANCHI

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Albert Chalamila, akizungumza wakati wa Mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam,  leo kuhusiana na Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika AGRF unaotarajia kuanza tarehe 5-8 Mwezi huu katika Kituo Cha Kimataifa Cha Mikutano  Cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Na: Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema kuwa wakazi wa Dar es Salaam wanapaswa kuchangamkia fursa zitakazotokana na mkutano wa Jukwaa la mfumo wa chakula la Afrika (AGRF), kwa lengo la kuongeza uzoefu na kujifunza teknolojia za kisasa ili kutimiza malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kulisha Dunia.

Aidha amewataka wakazi hao kudumisha usalama, ukarimu na usafi ili kuweka taswira nzuri ya Jiji la Dar es Salaam na nchi kwa ujumla.

Chalamila ameyasema leo Septemba 1, 2023 Jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza kwenye  mkutano na waandishi wa habari kuhusiana na Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF), unaotarajia kuanza tarehe 5-8 Mwezi huu katika Kituo Cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Jijini humo.

Amewataka wananchi kutumia fursa zitakazopatikana katika mkutano huo ili kuboresha shughuli za kilimo

“Mkutano huu utaleta matokeo muhimu katika uendelezwaji wa mifumo ya chakula Afrika , ukuzaji wa sekta ya Utalii, Biashara na Uwekezaji,  na kukuza teknolojia mpya” amesema Chalamila.

Naye, Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Ephrahim Mafuru, amesema Serikali inatatarajia kupokea wageni zaidi 3000 wa masuala ya kilimo, ambapo jumla ya sh. Bilioni 12.5 zimetolewa kwa ajili ya maandalizi ya mkutano huo.

“Mchango wa kituo katika mnyororo wa thamani hivyo Serikali kwa kushirikiana na AGRF imejipanga kwa bajeti ya Bilioni 12.500 na fedha hizo ni maandalizi ya mkutano ambazo zitaingia katika mnyororo wa thamani wa maandalizi na gharama za kuuendesha mkutano huo,”amesema.

Jukwaa la mfumo wa chakula la Afrika (AGRF) ni jukwaa kuu la kilimo linalowakutanisha wadau mbalimbali wa Sekta ya Kilimo ili kujadili na kuchukua hatua za kiutendaji katika kuboresha njia za upatikanaji na usalama wa chakula na lishe kwa ujumla.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here