Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza kwenye Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam tarehe 07 Septemba, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza kwenye mjadala wa masuala ya Kilimo na Vijana wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam tarehe 07 Septemba, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amezitaka nchi za Afrika kutumia wakati huu wa changamoto nyingi duniani kuwa fursa kwa kufanya mageuzi ya sera na mifumo ya kilimo katika nchi zao.
Rais Samia amewataka viongozi wa Afrika kufanya tathmini ya vipaumbele na kuwawezesha vijana kuzalisha kulingana na mahitaji ya dunia ili kufikia mageuzi ya chakula na kuifanya sekta ya kilimo kuwafikisha katika Afrika tunayoitaka.
Rais Samia amesema hayo leo wakati akihutubia katika Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika (AGRF) lililofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC).
Aidha, Rais Samia amesema bara la Afrika limeendelea kuwa na uzalishaji duni wa chakula huku wananchi wakikabiliwa na njaa na magonjwa yanayohusiana na lishe licha ya kuwa na rasilimali zinazofaa kutumika katika kilimo.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amesema Serikali ya Tanzania imeanza kutekeleza ajenda 10/30 inayolenga kuongeza ukuaji wa sekata ya kilimo hadi 10% ifikapo mwaka 2030 ikilinganishwa na bajeti ya hivi sasa.
Rais Samia pia amesema Tanzania inayo fursa ya kuwa mzalishaji na msafirishaji mkubwa wa mazao ya nafaka, mbogamboga na mafuta ya kula kwa nchi za Afrika na dunia kwa ujumla.
Awali akizungumza katika mjadala wa masuala ya kilimo na vijana, Rais Samia amesema Tanzania inatumia TEHAMA katika kilimo kwa kuwekeza kwenye tafiti, kuwawezesha maafisa ugani kuwa na nyenzo, kuhifadhi chakula, na kutumia mbegu za kisasa.
Zuhura Yunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu