WIZARA ya Afya imetolea ufafanuzi taarifa za upotoshaji kupitia clip (video) iliyosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu gharama za uchangiaji bima ya Toto Afya.
Katika katika taarifa hiyo, Wizara imefafanua:
“Huu ni Upotoshaji- Hakuna sehemu Waziri wa Afya Mhe Ummy Mwalimu ameandika au kutamka kuwa gharama ya kuchangia Bima ya Toto Afya Kadi imeongezeka.
“Wanaosema hivyo ni Wapotoshaji na wanafanya propaganda katika jambo hili nyeti linalohusu Bima ya Afya.
“Wizara inapenda kusisitiza tena kuwa gharama ya Bima ya Afya ya Toto Afya Kadi ni ile ile 50,400/- kwa mwaka kwa mtoto.
Sasa watoto wasajiliwe mashuleni au kwenye vituo vya kulelea watoto. Lengo la hatua hii ni kuingiza watoto wengi zaidi kwenye bima hii ili fao hili liwe endelevu na stahamilivu.
Hadi sasa Bima ya Afya ni hiyari. Tutaendelea kutoa elimu na hamasa ili wazazi/walezi wengi zaidi wawakatia watoto wao bima ya Afya ili kuwa na uhakika wa matibabu mwaka mzima.
Tunaendelea kutoa rai kwa wananchi kujiunga na bima ya Afya kwa wingi wao kwani kadri watu wengi wakijiunga na Bima ndio gharama za uchangiaji pia zinaweza kupungua na pia mafao zaidi yanaweza kupatikana huku tukijihakikishia Uhai na Uendelevu wa Fao hili.
Mwisho kabisa Mhe Ummy Mwalimu siyo Waziri wa Elimu kama mtu huyu anavyosema hapa, tunawaomba mpuuzie taarifa hii na kufuata taarifa rasmi kwenye vyanzo husika vya taarifa kupitia kurasa za NHIF na Wizara ya Afya mtandaoni.
Tusifanye Upotoshaji au Propaganda kuhusu Jambo hili.” ilimalizia taarifa hiyo kutoka Wizara ya Afya.