NA: JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM
Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Kimataifa Cha Mikutano cha Arusha (AICC) Bw. Ephrahim Mafuru amesema kuwa wapo katika mipango na mikakati ya kufanya maboresho katika maeneo mbalimbali ya make majengo yake ya mikutano ikiwemo kufanya uwekezaji ili kuleta tija na maendeleo kwa Taifa.
Miongoni mwa uwekezaji unaotarajia kufanyika ni kujenga Kituo Kikubwa cha Kisasa cha kuendesha Utalii wa Mikutano Cha Mount Kilimanjaro International Convention Centre (MKICC) Jijini Arusha.
Akizungumza na Mwandishi wa Full Shangweblog leo Septemba 2, 2023 Jijini Dar es Salaam Bw. Mafuru, amesema kuwa hiki kitakuwa kituo cha Kisasa cha Mikutano MKICC ambacho wanatarajia kujenga kitakachokuwa na uwezo wa kuchukua watu 3,000.
Bw. Mafuru amesema kuwa Kituo cha MKICC kitaweza kufanya maonesho kwa watu 10,000 jambo ambalo ni rafiki kwa maendeleo ya uchumi wa utalii wa mikutano Tanzania.
“Ni fursa ya uchumi wa mikutano ambayo itatusaidia kushiriki katika mnyonyoro wa thamani” amesema Bw. Mafuru.
Amesema kuwa pia watajenga hoteli mbili za nyota Tano na Nne pamoja na maeneo maalamu kwa ajili ya kutoa huduma kwa viongozi Wakuu wa Kitaifa.
Bw. Mafuru amesema kuwa uchumi wa mikutano bado upo nyuma, hivyo ni fursa kwao kuwekeza kwa kujenga vituo vya kisasa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Zanzibar na Dodoma.
“Leo hii ukiwa na Marais 20 Jijini Arusha na wasaidizi wao watalala wapi ? tunakwenda kujenga Hoteli za kisasa katika maeneo rafiki ya kulala marais kutoka nchi mbalimbali Duniani” amesema Bw. Mafuru.
Amesema kuwa wanaiangalia jijini la Dodoma pia kama Makao Makuu, Zanzibar yenye utalii mkubwa ili kuhakikisha uchumi wa mikutano bado unafikiwa na kuongeza fursa za uwekezaji nchini.
Pia wanatarajia kuboresha Hospitali ya AICC ili wadau mbalimbali waweze kupata huduma ya afya, huku akieleza kuwa awali ilikuwa hospital ya rufaa lakini kwa sasa imepitwa na hospitali nyingi hivyo kuna kila sababu ya kuinoresha zaidi hospitali hiyo.
Hata hivyo Bw. Mafuru amesema kuwa wanakwenda kubadilisha matumizi ya viwanja ambavyo vipo jijini Arusha kwa kujenga nyumba za kisasa ili waweze kujiendesha kibiashara.
“Maeneo mengine ikiwemo Uzunguni unakuta nyumba inakiwanja cha mita za mraba 4, 000 bei inayolipwa ni robo ya bei ya soko, kuna watu ni madalali wa nyumba za AICC tunakwenda kudili nao ili kiwatoa katika mchezo huo” amesema Bw. Mafuru.
Amesema kuwa lengo ni kujenga nyumba za kisasa ambazo wanakwenda kupangisha na kuuza kwa bei ya soko.
“Tumeshatangaza katika mfumo wa manunuzi ya serikali mpango kanambe wa viwanja vyetu, nachukua fursa hii kuwatangazia watanzania wenye nia njema na kuomba kutengeneza ramani ya AICC mpya” amesema Bw. Mafuru.
Amesema kuwa wakati umefika kwa viongozi wa serikali pamoja na wadau mbalimbali wanapokwenda kushiriki mikutano nje ya nchi kuitangaza Tanzania ili tuweze kupata fursa ya kuwa wenyeji wa mikutano mbalimbali ya Kimataifa.
“Wanapokwenda katika mikutano nje ya nchi kuiwakilisha nchi mfano Madaktari wahandisi wanapaswa kutia neno la kuwakaribisha Tanzania na kutangaza fursa za uwekezaji ikiwemo mbuga za wanyama” Na kukaribisha mikutano mikubwa ya kimataifa amesema Bw. Mafuru.
Amesema kuwa ushirikiano wa Taasisi mbalimbali katika kuitangaza nchi Kimataifa itasaidia kuvutia mikutano mingi kutoka nchi mbalimbali Duniani kufanyika nchini Tanzania.
Katika hatua nyengine amebainisha kuwa ipo mipango ya kuboresha Kituo cha mikutano Cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) ili kiwe na uwezo wa kuchukua watu 3,000 kwa wakati mmoja.
Bw. Mafuru ameeleza kuwa hivi karibuni kulikuwa na mkutano wa Afya ambapo Tanzania ilishirikiana na Chama cha Madaktari wa meno wakristo Duniani na kushirikisha watu 1,000 kutoka nje ya nchi.
“Ni mkutano mkubwa haujawahi kufanyika Afrika, ni mara ya kwanza kufanyika nchini Tanzania ambapo ulikuwa na fursa nyinyi” amesema Bw. Mafuru.
Amesema kuwa wageni walipata nafasi ya kutembelea hospitali na baadhi ya taasisi zinazoshiriki katika sekta ya afya.
Bw. Mafuru amesema kuwa kituo kina mipango mingi yenye kuleta tija, huku akibainisha wamefanikiwa kupata faida kwa mwaka huu kwani awali walikuwa wanajiendesha kwa hasara kwa zaidi miaka ya miaka mitano.
Hata hivyo ameeleza kuwa mpaka sasa wanadai shilingi bilioni saba na kuwakumbusha Wakuu wa Taasisi mbalimbali pamoja Mashirika mbalimbali wanaodaiwa kulipa madeni ili fedha zitakazopatikana ziweze kusaidia kufanya uwekezaji waTaasisihiyo.