Home LOCAL MIAKA 20 YA PEPFAR: KITUO CHA BIKIRA MARIA MAMA WA TUMAINI –...

MIAKA 20 YA PEPFAR: KITUO CHA BIKIRA MARIA MAMA WA TUMAINI – MASANGA KIMBILIO SALAMA LA TOHARA

Msimamizi wa kituo cha Afya cha Bikra Maria Mama wa Tumaini (BMMT) na Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya ATFGM,  Sister Jacqueline Gbanga akielezea namna wanavyoshirikiana na PEPFAR kukabiliana na Maambukizi ya VVU kupitia Tohara Kinga ya Kitabibu kwa Wanaume
 
Na: Kadama Malunde – Malunde 1 blog
  
Kituo cha Bikra Maria Mama wa Tumaini kilichopo katika Kijiji cha Masanga kata ya Goronga Halmashauri ya Tarime Mkoani Mara kimeeleza kupata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) kwa kutoa bure huduma ya kitabibu kwa wanaume wanaokimbia tohara ya kimila ili kupunguza maambukizi ya VVU.
 
Akizungumza Jumatano Agosti 16,2023 na Waandishi wa Habari wanaofanya ziara mkoani Mara, Msimamizi wa kituo cha Afya cha Bikra Maria Mama wa Tumaini (BMMT) na asasi ya ATFGM inayopinga ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike, Sister Jacqueline Gbanga amesema Kituo hicho kimekuwa kikitumika kama hifadhi ya wanaume waliokimbia tohara ya kimila wakiwa na uhitaji wa kufanya tohara ya kitabibu.
 
 
Amesema Kituo hicho kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma Mkoa wa Mara na kusimamiwa na Daughters of Charity of Vincent de Paul kinatumika kama hifadhi ya wanaume waliokimbia tohara ya kimila wakiwa na uhitaji wa kufanya tohara ya kitabibu kwa sababu ya usalama na kuepuka utokwaji wa damu, maambukizi yanayotokana na kifaa kimoja cha tohara, maumivu makali na wakati mwingine vifo.
 
Sr. Jacqueline ameeleza kuwa tangu waanzishe huduma ya tohara mwaka 2018 jumla ya vijana na wanaume 88 waliokimbia huduma za tohara ya kimila wamepata huduma ya tohara ya kitabibu bure katika kituo hicho kwa njia ya huduma mkoba ya tohara (Informed facility led outreach).
Msimamizi wa kituo cha Afya cha Bikra Maria Mama wa Tumaini (BMMT), Sister Jacqueline Gbanga akisoma taarifa kuhusu Tohara Kinga ya Kitabibu kwa Wanaume
 
Amebainisha kuwa kwa kushirikiana na hospitali ya wilaya ya Nyamwaga inayotoa huduma endelevu za tohara, wamefanikiwa kupata watoa huduma pamoja na vifaa tiba ikiwa ni ushirikiano mkubwa unaotolewa na Shirika la Amref Health Africa Tanzania linalopata ufadhili wa PEPFAR kupitia CDC.
 
“Tunapoadhimisha miaka 20 toka tulipoanza kupata msaada kutoka Serikali ya Marekani kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa kupambana na UKIMWI (PEPFAR) kwa ajili ya kupigana na janga la VVU/UKIMWI, tunashukru sana kwa maana bila msaada wenu tusingeweza kufanikisha Tohara kinga ya kitabibu. Tunashukuru vijana wamepata na wanaendelea kufanyiwa tohara ya kitabibu”,amesema Sr. Jacqueline.
 
“Mchango wa PEPFAR kupitia CDC, kwa kushirikiana na Amref pamoja na Wizara ya Afya vimeongeza tumaini kwa wananchi ambao pia ni maskini wasiokua na uwezo wa kipato kwa ajili ya gharama za matibabu lakini wanapata huduma zote bure katika kituo hiki”,ameongeza.
 
Katika kupinga mila kandamizi kwa watoto ikiwemo ukeketaji na tohara ya jadi ambayo haizingatii afya ya mtu, Sr. Jacqueline amesema kituo hicho kimekuwa kikihamasisha makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, wazee wa mila, wachungaji, walimu, watalamu wa afya, watu maarufu katika jamii, viongozi wa vijiji na vitongoji na serikali kuendelea kuhamasisha tohara kinga ya kitabibu (VMMC) kuweza kupunguza maambukizi ya VVU.
 
“Mila hii ya tohara kwa Wakurya zimejenga hofu kwa watoto na vijana. Tunaendelea kupiga vita mila kandamizi kukeketa watoto wa kike na kulazimisha watoto wa kiume kutahiriwa bila ganzi na kupata maumivu makali, kuvuja damu nyingi na hata kupelekea kupoteza uhai”,ameeleza.
Mratibu Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) Tanzania, Bi. Jessica Greene akizungumza katika kituo cha Afya cha Bikra Maria Mama wa Tumaini Masanga 
 
Mratibu Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI – The U.S. President’s Emergency Plan for AIDS Relief (PEPFAR) Tanzania, Bi. Jessica Greene amesema tohara kinga ya kitabibu inalenga kupunguza maambukizi ya VVU.
 
 
Ameongeza kuwa Serikali ya Marekani inaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kufikia malengo ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Kupambana na Ukimwi Duniani (UNAIDS) 95/95/95 (95% (ya watu wanaoishi na VVU wanajua hali zao, 95% ya waliogundulika wako kwenye matibabu, 95% ya wanaopata matibabu virusi vitakuwa vimefubazwa ifikapo 2025.
 
Mkurugenzi Msaidizi wa CDC Tanzania Dkt. George Mgomella amesema huduma za tohara kinga ya kitabibu Mkoani Mara zimekuwa zikifanyika kwa ushirikiano wa Serikali ya Marekani na Tanzania kupitia Amref Health Africa Tanzania inayotekeleza Mradi wa Afya Kamilifu kupitia CDC kwa ufadhili lengo likiwa ni kupunguza maambukizi ya VVU.
 
Naye Mhamasishaji wa tohara kinga ya kitabibu kutoka Kijiji cha Masanga, Mwalimu Baraka Joseph amesema Amref Health Africa Tanzania kupitia CDC kwa ufadhili wa PEPFAR wamesaidia kwa kiasi kikubwa vijana kuondokana na hali ya ukimbizi kwenye jamii yao wakikwepa tohara ya kimila.
 
“Tohara ya kimila imekuwa ikiwafanya wanaume kuwa wakimbizi kwenye jamii yao, tunashukuru katika eneo hili la Masanga na kata hii ya Goronga ambayo ilikuwa na Mangariba na wazee wengi wa mila elimu ya tohara ya kitabibu inazidi kusambaa na wanaume wameendelea kujitokeza kupata huduma hii bure”,amesema Mwl Joseph.
 
Mratibu wa Masuala ya UKIMWI Halmashauri ya Tarime ,Dkt. Rebeca Mngumi ameeleza kuwa kituo cha Afya cha Bikra Maria Mama wa Tumaini ni kati ya vituo 6 vinavyotoa huduma ya tohara kinga ya kitabibu katika halmashauri hiyo na kimekuwa msaada mkubwa katika kuwakomboa vijana dhidi ya tohara ya kimila.
 
“ Masanga kuna wazee wengi wanaofanya tohara za kimila katika wilaya ya Tarime, kutokana na hali hii tumekuwa tukitoa elimu ya tohara ya kitabibu katika jamii. Kipindi cha tohara za kimila ambazo hufanyika miezi ya Oktoba hadi Februari vijana wengi wamekuwa wakikimbilia kwenye kituo hiki ili kukwepa tohara hiyo isiyo salama kutokana na vifaa vinavyotumika kufanyia tohara”,amesema Dkt. Rebeca.
 
Kwa upande wake, Mhudumu Ngazi ya jamii, Rose Chikaka ambaye anafanya kazi ya uhamasishaji wa tohara nyumba kwa nyumba amesema huduma ya tohara kinga bure sasa inachangamkiwa na wanaume wengi wanaotoka kwenye jamii iliyoamini tohara ya kimila ambayo ilikuwa inawapotezea gharaa na muda mwingi kujiandaa kwa ajili ya shughuli tohara,kuwa hatarini kupata maambukizi ya VVU, kutokwa damu nyingi na wakati mwingine kifo.
Mhudumu Ngazi ya jamii, Rose Chikaka.
Naye mtoa huduma za tohara katika kituo cha BMMT ,Godfrey Mago amesema vijana wengi wanakimbilia huduma ya tohara kinga ya kitabibu ili kuepuka maumivu wakati wa tohara ya kimila, kupoteza muda mwingi na gharama za tohara za kimila mfano kutozwa sh. 25,000/= ili upatiwe huduma lakini pia kupigwa faini ya hadi sh. 30,000/= endapo utalia au kupiga kelele wakati ukifanyiwa tohara ya kimila.
 
 
“Nilitoroka nyumbani nikaja BMMT kufanyiwa tohara salama tofauti na tohara ya kimila ambayo hata kidonda kinachukua muda mrefu kupona. Naishukuru sana PEPFAR kwa kuleta huduma hii bure”,ameongeza Juma Magaiwa Msenda ambaye ni mnufaika wa huduma za tohara kinga ya kitabibu.
 
 
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Zabron Masatu amesema kupitia PEPFAR mpaka sasa wamefanikiwa kuwafanyia tohara kinga ya kitabibu wanaume wapatao 63,000 mkoani humo ambapo hayo yote yanatokana na uhamasishaji wa tohara ya kitabibu inayotolewa bure kwa wanaume ikiwa ni juhudi za kukabiliana na maambukizi ya VVU.
Msimamizi wa kituo cha Afya cha Bikra Maria Mama wa Tumaini (BMMT) na Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya ATFGM,  Sister Jacqueline Gbanga akisoma taarifa namna wanavyoshirikiana na PEPFAR kukabiliana na Maambukizi ya VVU kupitia Tohara Kinga ya Kitabibu kwa Wanaume. Kushoto ni Mratibu Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) Tanzania, Bi. Jessica Greene.
Msimamizi wa kituo cha Afya cha Bikra Maria Mama wa Tumaini (BMMT) na Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya ATFGM,  Sister Jacqueline Gbanga akisoma taarifa namna wanavyoshirikiana na PEPFAR kukabiliana na Maambukizi ya VVU kupitia Tohara Kinga ya Kitabibu kwa Wanaume.
Mratibu Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) Tanzania, Bi. Jessica Greene akizungumza katika kituo cha Afya cha Bikra Maria Mama wa Tumaini (BMMT). Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa CDC Tanzania Dkt. George Mgomella.
Mratibu Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) Tanzania, Bi. Jessica Greene akizungumza katika kituo cha Afya cha Bikra Maria Mama wa Tumaini (BMMT).
Waandishi wa habari wakichukua matukio katika kituo cha Afya cha Bikra Maria Mama wa Tumaini (BMMT).
Mkurugenzi Msaidizi wa CDC Tanzania Dkt. George Mgomella katika kituo cha Afya cha Bikra Maria Mama wa Tumaini (BMMT)
Mhamasishaji wa tohara kinga ya kitabibu kutoka Kijiji cha Masanga, Mwalimu Baraka Joseph akielezea kuhusu huduma ya tohara kinga ya kitabibu kwa wanaume
Mhamasishaji wa tohara kinga ya kitabibu kutoka Kijiji cha Masanga, Mwalimu Baraka Joseph akielezea kuhusu huduma ya tohara kinga ya kitabibu kwa wanaume
Juma Magaiwa Msenda ambaye ni mnufaika wa huduma za tohara kinga ya kitabibu akielezea kuhusu huduma ya tohara kinga ya kitabibu kwa wanaume
Mratibu wa Masuala ya UKIMWI Halmashauri ya Tarime , Dkt. Rebeca Mngumi akielezea kuhusu huduma ya tohara kinga ya kitabibu kwa wanaume
Mtoa huduma za tohara katika kituo cha BMMT ,Godfrey Mago akielezea kuhusu huduma ya tohara kinga ya kitabibu kwa wanaume
Bango katika kituo cha Afya cha Bikra Maria Mama wa Tumaini (BMMT)
Viongozi wakipiga picha ya kumbukumbu katika kituo cha Afya cha Bikra Maria Mama wa Tumaini (BMMT).
 
Picha na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here