Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse akizungumza katika Mkutano uliojumuisha Ofisi ya Msajili wa Hazina, STAMICO, na wahariri wa Vyombo vya habari, uliofanyika leo Agosti 28,2023 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile akifuatilia wasilisho la Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse katika Mkutano wa Taasisi hiyo na Wahariri wa Vyombo vya habari, kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, akizungumza alipokuwa akitoa neno kwa niaba ya Wahariri waliohudhuria katika mkutano huo, uliofanyika leo Agosti 28, 2023 Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
(PICHA ZOTE NA HUGHES DUGILO)
Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM
Shirika la Madini la Taifa-STAMICO, limefanya mageuzi makubwa kwa kuongezeka mapato ya ndani kutoka shilingi Bilioni-1.3 mwaka 2018/2019 hadi kufikia shilingi Bilioni-61.1 kwa mwaka 2022/2023.
Mafanikio hayo yametangazwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse, katika mkutano uliojumuisha Ofisi ya Msajili wa Hazina, STAMICO, na wahariri wa Vyombo vya habari uliofanyika leo Agosti 28,2023 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
Mafanikio mengine ya Shirika hilo lenye umri wa miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, yanatajwa ni kutoka Shirika linalotengeneza hasara hadi Shirika linalotengeneza faida na hatimaye kuweza kulipa Gawio Serikalini.
“STAMICO imepata mafanikio makubwa ambapo tumefanikiwa Kutoka Shirika linalotengeneza hasara hadi Shirika linalotengeneza faida, tumeweza kulipa gawio kwa serikali jumla ya Shilingi Bilioni 8, tumeondokana kabisa na utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini, tumepata hati safi kwa miaka 3 Mfululizo kutokana na ukaguzi wa Mahesabu, lakini pia Mapato ya ndani yameongezeka kutoka Shilingi Bilioni 1.3 kwa Mwaka 2018/19 hadi Shilingi Bilioni 61.1 kwa mwaka 2022/23.” Amefafanua Dkt. Mwasse.
Aidha, Shirika hilo linalotarajia kujiendesha bila ruzuku ya serikali, katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, limeanza kuzalisha Mkaa wa kupikia kwa kutumia Makaa ya Mawe yaliyopo Kiwira-Kabulo.
Pia Mkurugenzi Mkuu wa Stamico, amesema wanakusudia kuanzisha Benki ya wachimbaji wadogo ikilenga kuwaondokana kero ya kutokopesheka kwenye Mabenki na itawasaidia kukuza mitaji na uchumi wao.
Katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo, Dokta Mwasse, amesema Stamico imenunua mitambo mitano ya kufanya uchorongaji na kwamba mitambo hiyo inatarajiwa kufika nchini mwezi Septemba mwaka huu.