Na: Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM
Wakala wa majengo Tanzania (TBA) imedhamiria kutoa auheni na suluhisho la uhaba wa nyumnba za makazi ya watu kote nchini, kwa wananchi ambao sio watumishi wa umma.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Mawasiliano na Masoko TBA, Fredrick Kalinga katika mahojiano na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa lengo ni kujenga nyumba elfu kumi, kwa ajili ya watumishi wa umma nchi nzima, lakini pia kuna matumaini mapya kwa ajili ya watu wasio watumishi wa umma.
Matumiani haya yamekuja baada ya nia njema ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alipotoa maelekezo wakati akifungua nyumba za Magomeni Kota kwamba, Sheria ambayo alianzisha wakala wa Majengo (TBA) iweze kubadilishwa ili kupata nafasi ya kushirikiana na Sekta Binafsi katika kutekeleza majukumu yake ya ujenzi wa nyumba.
“Mara baada ya kupokea maelekezo hayo na kuyafanyia kazi maboresho hayo, tayari yameshafikia katika hatua nzuri.
“Sisi tumefenya eneo letu, na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ipo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha maboresho ambayo tumeyafanya kwenye Sheria ya uanzishaji wa Wakala ili sasa tuweze kuwa na ushirikiano na Sekta Binafsi.
“Hii itatusaidia kuweza kuendeleza maeneo ambayo sisi TBA tunayamiliki katika maeneo mbalimbali, na hapo sasa tutapata nafuu ya kuwapangisha watu ambao siyo watumishi wa umma, na kama tutajenga kwa ajili ya kuuza, tutauza hata kwa ambao sio watumishi wa umma. Kwa hiyo, kwa pamoja tutaweza kupunguza wimbi la watu wasio na makazi hapa nchini” amesema Kalinga.