Na: Neema Adriano
Naibu Waziri Wizara ya fedha na mipango Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir amebainisha kuwa Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano kwa kila mwenye nia ya kuwekeza visiwani humo kutokana na uwepo wa fursa mbalimbali zilizopo za Uwekezaji.
Mhe. Ameir meyasema hayo katika hafla maalum ya siku ya Zanzibar iliyoadhimishwa Julai 12, 2023, katika maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), kwenye Viwanja vya Mwalimu Juliaus Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeamua kufungua milango ya kimaendeleo na kwamba, imekuwa ikipanga na kutekeleza mikakati mbalimbali katika kuleta mabadiliko kwenye Sekta ya Utalii, Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
“Kila ambaye ana nia ya kuwekeza tutashirikiana nae, tumeamua kuhakikisha tunawawezesha wajasiliamali wa Zanzibar, tumeamua kufungua Zanzibar kimaendeleo, na Serikali imekuwa ikipanga na kutekeleza mikakati mbalimbali katika kuleta mabadiliko katika sekta ya utalii, Viwanda Biashara na Uwekezaji,”
“Madhumuni ni kuitangaza Zanzibar katika fursa zilizopo ikiwemo kibiashara, hasa kwenye uchumi wa buluu, na Uwekezaji, na kuutangza utamaduni wetu” amesema Mhe. Ameir.
Ameongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefanya maboresho makubwa kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kuimarisha huduma za Viwanja vya ndege, sambamba na kuimarisha huduma za mizigo, kuimarisha na kuanzishwa kwa Bandari kavu, uwanja wa maonesho, na Viwanda vidogo vidogo.
Aidha amewakaribisha watu wote kutembelea Zanzibar kutokana na historia yake ambapo pamoja na mambo mengine, watapata fursa ya kujionea mambo mbalimbali yaliyopo visiwani humo ikiwemo na utalii.