Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Omar Juma Kipanga (kulia), akimsikiliza Mratibu wa mafunzo wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania, Bi. Agnes Chihoma, alipokuwa akitoa maelezo kuhusiana na Chuo hicho, wakati kiongozi huyo alipotembelea Banda lao, katika Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyomalizika rasmi leo Julai 22,203, kwenye viwanja vya Mnazi mmoja Jijinidar es Salaam.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Omar Juma Kipanga (kushoto), akizungumza jambo na Mratibu wa mafunzo wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania, Bi. Agnes Chihoma, (kulia), wakati Kiongozi huyo alipofanya ziara ya kukagua mabanda ya washiriki, kwenye Maonesho hayo. (katikati), ni Katibu Mtendaji, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, (TCU) Prof. Charles Kihampa.
Mratibu wa mafunzo wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania Bi. Agnes Chihoma, (kushoto), akizungumza na wanafunzi wa Sekondari waliotembelea banda la Chuo hicho kwenye Maonesho hayo.
(PICHA NA: Mpiga picha maalum)
Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.
Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania cha Jijini Mwanza, kimepata mwitikio mkubwa wa wanafunzi waliotembelea katika Banda la Chuo hicho, kwenye Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyofungwa rasmi leo Julai 22,203, katika viwanja vya mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa maonesho hayo yaliyoratibiwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Mrtibu wa mafunzo wa Chuo hicho Bi. Agnes Chihoma, ameeleza kuwa kumekuwepo na mwitikio mkubwa wa wanafunzi kutaka kufahamu fursa za masomo, sambamba na kufanya udahili wa papo kwa hapo, ambapo zaidi ya watu 500 wametembelea Banda lao.
“Chuo cha Benki kuu ya Tanzania, kilichopo Capripoint Jijini Mwanza ni chuo chenye ithibati ya baraza la taifa la elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi yaani NACTVET, chuo kinatoa stashahada ya taaluma ya kibenki na usimamizi wa mabenki yaani Ordinary Diploma in Banking Practice and Supervision na stashahada ya uzamili katika uongozi wa benki yaani Postgraduate Diploma in Bank Management.”
“Sifa za kujiunga na programu ya Diploma ni angalau ufaulu wa principal pass moja na subsidiary pass moja kwa kidato cha sita au cheti cha ufundi Daraja la nne (National Technical Award Level 4) katika taaluma yoyote ya biashara kutoka chuo kinachotambuliwa na NACTVET”
“Kwa upande wa Postgraduate Diploma, Programu hii inaendeshwa katika vyumba vya mafunzo vilivyopo Benki Kuu makao makuu ndogo Dar es Salaaam” ameeleza Bi. Chihoma.
Ameongeza kuwa, Chuo hicho pia kinatoa mafunzo ya muda mfupi kwa watu waliopo katika taasisi za fedha. Lengo la mafunzo haya ni kuwapa ujuzi na kuongeza ufanisi wa utendaji wao wa kazi..
Ratiba ya mafunzo hayo inatoka kila mwaka mwezi wa kumi na moja, na inapatikana katika website ya chuo ambayo ni academy.bot.go.tz.
Aidha mwanafunzi anaweza kutuma maombi yake ya kujiunga na Chuo hicho popote alipo, na maombi yanapokelewa kupitia mfumo wa maombi wa chuo ambao ni https://oas.botac.ac.tz.
Maonesho hayo yenye kaulimbiu isemayo, “Kukuza ujuzi nchini kupitia Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kwa uchumi imara na shindani” yameshirikisha Vyuo na Taasisi za Elimu ya Juu zaidi ya 80 ambapo, yalifunguliwa rasmi Julai 18 mwaka huu, na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb)