Home LOCAL WABUNGE WAJIPANGA KUIMARISHA USTAWI WA JAMII NCHINI

WABUNGE WAJIPANGA KUIMARISHA USTAWI WA JAMII NCHINI

Na: WMJJWM, DODOMA

Wabunge Vinara wa Huduma za Ustawi wa Jamii wametaka huduma hizo zipatikane katika maeneo na taasisi za kijamii ikiwemo Bungeni.

Wabunge hao wamesema hayo wakati wa kikao chao cha siku mbili na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum chenye lengo la kuelimisha Wadau na kupokea maoni kuhusu jinsi ya kuimarisha na kuboresha utoaji wa huduma za ustawi wa Jamii nchini, Juni 25 – 26, 2023.

Baadhi ya wabunge waliochangia hoja katika kikao hicho, wengi wao wameishauri Serikali kuhakikisha changamoto ya uhaba wa Maafisa Ustawi wa Jamii inapatiwa ufumbuzi kutokana na mahitaji makubwa ya huduma hizo kwa zama za sasa.

“Maeneo ya pembezoni yaangaliwe pia katika huduma za ustawi wa jamii, kwa mfano mkoa wa Lindi bado kuna uhaba wa maafisa ustawi wa jamii na hasa kipindi hiki ambapo athari za mambo mengi zinaleta tatizo la afya ya akili hivyo, maafisa hawa wanatakiwa kusaidia watu” amesema Mhe. Tekla Ungele.

Naye Mbunge wa Manyoni Mashariki Mhe. Dkt.Pius Chaya ameeleza kuwa Huduma za Ustawi wa Jamii zimejikita zaidi kwenye Vituo vya Afya kuliko kwenye jamii ambapo ameshauri Maafisa Ustawi wa Jamii wapatikane pia ndani ya jamii.

Aidha, katika kikao hicho kilichohusisha pia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, wabunge wameshauri kuwa na mpango mzuri wa kuwekeza kwenye akili za watoto wadogo kuanzia ngazi ya awali ili kutengeneza jamii iliyoimarika hapo baadaye.

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amebainisha kuwa, tayari Ofisi ya Rais TAMISEMI imeshazielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha zinajadili kwenye vikao vyote vya Halmashauri masuala yote yanayohusu huduma za Ustawi wa Jamii ikiwemo masuala ya maadili na vita dhidi vitendo vya ukatili.

Ameongeza kuwa, ajenda hiyo inatakiwa kujadiliwa kwa umuhimu wake kama ilivyo kwa Ajenda nyingine za maendeleo.

“Tutafuatilia kweli kila robo mwaka kama maelekezo haya yamefanyiwa kazi kwenye vikao vyote hadi hiyo ‘Full Council’ kwa sababu wasipoongea huko chini hakuna kitu kitaendelea huku ngazi ya juu” amesema Waziri Dkt. Gwajima.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here