Home LOCAL UTAWALA BORA, SHERIA BORA NDIO MSINGI WA MAENDELEO YA UCHUMI – DKT....

UTAWALA BORA, SHERIA BORA NDIO MSINGI WA MAENDELEO YA UCHUMI – DKT. SAMIA

Na: Magdalena Nkulu , WMJJWM, DODOMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inazingatia Utawala Bora na Utawala wa Sheria kwa vile inaelewa kuwa hayo yote ni msingi wa maendeleo ya uchumi.

Akizungumza kwa niaba yake katika Mkutano wa Sita wa Maombi ya Kitaifa chini ya Shirika la KINGDOM NETWOK LEADERSHIP Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema Mkakati wa Maendeleo wa Kitaifa wa Miaka Mitano umesisitiza Utawala Bora na Utawala wa Sheria kama msingi wa maendeleo ya kiuchumi.

Amesema kupitia kaulimbiu ya mwaka huu ya mkutano huo, inayosema “Nguvu ya Tabia katika Uongozi” anaamini kwamba Taifa haliwezi kujengwa bila uongozi wenye uadilifu, maadili na maadili, hivyo watu wanapofanya kazi kwa uadilifu na kuwathamini wengine, kila mtu hupokea huduma zinazostahili kwa wakati na anaridhika.

“Tunahitaji uadilifu katika ukusanyaji wa kodi na mapato, usimamizi wa fedha za umma na uwajibikaji. Tunahitaji uadilifu katika uwekezaji na katika kushughulika na wawekezaji. Nimefurahia kuona kwamba KLNT imeweka pamoja mkutano huu wa Sala ya Kitaifa”

Waziri Dkt. Gwajima ameongeza kwamba Matukio kama hayo ya kukutana na kuomba Mungu, yanasaidia kwa Maendeleo ya Taifa kwani ni fursa ya kuwekana sawa kwa faida ya Taifa na kutoa wito yafike hadi ngazi ya chini kupitia uratibu wa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste (CCT), Askofu Stanly Hotay amewasihi viongozi kutafuta hekima zaidi na kujitoa kuwajali wengine na kuwa waadilifu.

“Unaweza ukawa na nafasi, nguvu na uwezo lakini ukaangushwa na tabia yako, tabia ndio msingi wa yote. Sifa namba moja ya mtu wa tabia njema ni upendo” amesema Askofu Hotay.

Naye Mratibu wa kongamano hilo Isack Mpandwa amebainisha malengo ya Maombi hayo ya Taifa ambayo yanafanyika kwa mara ya sita mwaka huu kuwa ni kuliombea Taifa, kumshukuru Mungu na kuwaombea viongozi wa kitaifa.

Viongozi wengine waliohudhuria Mkutano huo ni Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe. Balozi Pindi Chana, Mbunge wa Jimbo la Nsimbo Mhe. Anna Lupembe, Mbunge viti Maalum Mhe. Ritha Kabati na Mbunge wa Serengeti Mhe. Amsabi Mrimi.

Wengine ni wageni kutoka nje ya nchi Profesa Patrice Lumumba kutoka Kenya, Mchungaji Dkt. Paul Enenche kutoka Nigeria na Mfanyabiashara maarufu Lloyd Ward.

MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here