Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Mhe.Dkt.Tulia Ackson, Mkuu wa Mkoa Dodoma Rosemary Senyamule pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela kuongoza Matembezi ya Wabunge na Watumishi wa Bunge kuelekea katika Tamasha la Bunge Grand Bonanza lililofanyika katika Shule ya Sekondari ya John Merlin Jijini Dodoma leo tarehe 24 Juni 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Mhe.Dkt.Tulia Ackson, Mkuu wa Mkoa Dodoma Rosemary Senyamule, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela, Wabunge na Watumishi wa Bunge wakiwasili katika Shule ya Sekondari ya John Merlin Jijini Dodoma kushiriki Tamasha la Bunge Grand Bonanza leo tarehe 24 Juni 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa wakishuhudia michezo mbalimbali inayochezwa na Wabunge pamoja na Watumishi wa Bunge wakati wa Tamasha la Bunge Grand Bonanza lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlin Jijini Dodoma leo tarehe 24 Juni 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikagua timu ya Wabunge na Watumishi wa Bunge kabla ya kuanza kwa mechi ya mpira wa miguu baina ya timu hizo wakati wa Tamasha la Bunge Grand Bonanza lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlin Jijini Dodoma leo tarehe 24 Juni 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikagua timu ya Wabunge na Watumishi wa Bunge kabla ya kuanza kwa mechi ya mpira pete baina ya timu hizo wakati wa Tamasha la Bunge Grand Bonanza lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlin Jijini Dodoma leo tarehe 24 Juni 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikabidhi Kombe kwa washindi wa Jumla wa Tamasha la Bunge Grand Bonanza ambao ni Waheshimiwa Wabunge walioshinda dhidi ya Watumishi wa Bunge mara baada ya kumalizika kwa michezo mbalimbali iliofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlin Jijini Dodoma leo tarehe 24 Juni 2023.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania……!! Bunge Grand Bonanza Oyeee!!Awali ya yote, tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kushiriki kwenye Tamasha hili la michezo lijulikanalo kama “Bunge Grand Bonanza”. Aidha, nawaletea salaam kutoka kwa mwanamichezo namba moja, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anawatakia heri katika tamasha hili na mashindano mema yatakayosaidia kujenga afya zenu na pia kuimarisha ushirikiano miongoni mwenu. Nimefurahi sana kuona mwitikio mzuri na ushiriki mkubwa kwenye bonanza hili. Hii inadhihirisha kuwepo kwa mwamko mkubwa wa Wabunge na Watumishi wa Ofisi ya Bunge kwa ujumla wa kupenda na kuthamini michezo. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge mliopo, Ndugu Washiriki; Kipekee kabisa, naomba nikushukuru sana Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kunialika kuwa Mgeni rasmi na pia kushiriki katika tamasha hili. Aidha, nakupongeza wewe na Uongozi mzima wa Bunge kwa kuandaa michezo hii inayotuleta pamoja kwa ajili ya kuburudika, kujenga na kuimarisha afya, kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kibunge, kujenga umoja na urafiki miongoni mwetu na kuhamasisha Watanzania wa rika zote kupenda michezo. Nimefurahishwa pia na kaulimbiu ya tamasha hili isemayo “Tupende Michezo, Tujenge Taifa letu”. Hii ni kaulimbiu muafaka kwa kuwa inalenga kutoa msisitizo juu ya umuhimu wa michezo na faida zitokanazo na michezo. Aidha, nimefurahi kuona kwamba tamasha hili litahusisha michezo ya aina mbalimbali, jambo ambalo linatoa nafasi kwa kila Mbunge kushiriki ipasavyo. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge mliopo, Ndugu Washiriki; Napenda pia nimshukuru sana Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Bwana Abdulmajid Nsekela kwa kudhamini tamasha hili. Aidha, naupongeza Uongozi mzima wa Benki ya CRDB, wanahisa, Bodi ya Wakurugenzi, Wadhamini, Wafanyakazi wa Benki hii pamoja na wadau wote kwa kufanikisha udhamini wa tamasha. Nawashukuru kwa dhati Benki ya CRDB kwa ubunifu huu wa kuandaa au kudhamini matamasha mbalimbali ya michezo yanayoandaliwa kwa malengo maalum. Ujenzi wa Taifa letu si jukumu la Serikali pekee bali ni la kila mdau. Benki ya CRDB imejipambanua kuwa kweli ni mdau wa maendeleo nchini. Hili linadhihirishwa kwa namna Benki inavyojihusisha kwa karibu na shughuli mbalimbali za kuwaletea wananchi maendeleo. Tumeshuhudia hivi karibuni mkiandaa Mbio za Marathon kwa ajili ya kuchangia huduma mbalimbali za jamii kama vile huduma kwa akina mama wenye ujauzito hatarishi, ununuzi wa madawati n.k. Asanteni sana. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge mliopo, Ndugu Washiriki; Mazoezi ya mwili ni muhimu sana kwa afya njema. Aidha, ujenzi wa nchi yetu unahitaji nguvukazi yenye afya njema. Hata hivyo, Watanzania wengi, hususan wanaoishi mijini, wanakabiliwa na hali ya uzito uliozidi na viribatumbo (overweight/obesity). Inasikitisha kuona kuwa vijana wengi siku hizi wanapoteza maisha kutokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari na shinikizo la damu; magonjwa ambayo kwa kiasi kikubwa husababishwa na mtindo wa maisha, ulaji usiofaa na kutofanya mazoezi mara kwa mara. Ni wakati muafaka sasa kupinga kwa nguvu zote tabiabwete ili kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kujenga tabia ya kufanya mazoezi. Shirika la Afya Duniani (WHO) limeitaja tabiabwete (physical body inactivity) kuwa ndicho kihatarishi kikubwa kinachosababisha magonjwa sugu na vifo ikifuatiwa na ulaji usiofaa na matumizi ya tumbaku. Kwa ujumla, magonjwa yasiyoambukizwa kwa sasa yanachangia takriban asilimia 60 ya vifo vya mapema kwa kila mwaka. Tabiabwete pia ni chanzo cha vifo takriban milioni 2.2 kila mwaka duniani kote na pia chanzo cha asilimia 15 hadi 20 ya magonjwa ya moyo, kisukari na aina kadhaa za kansa. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, hatari ya kupata magonjwa ya moyo inaongezeka mara 1.5 miongoni mwa watu wasiofuata utaratibu wa kufanya mazoezi unaopendekezwa kiafya. Duniani hivi sasa, inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watu wazima hawafanyi mazoezi ya kutosha kwa ajili ya afya zao. Mheshimiwa Spika na Ndugu Washiriki; Michezo imebainika kuwa na nafasi kubwa katika kukuza uchumi duniani kote. Tafiti zinaonesha kuwa michezo inachochea kukua kwa uchumi. Mathalan, ujenzi wa miundombinu ya michezo, kushamiri kwa sekta ndogo ya burudani na uzalishaji wa vifaa vya michezo ni chanzo kikubwa cha ajira na mapato. Zaidi ya hayo, michezo ni kichocheo cha ukuzaji maarifa hususan kwa vijana na hivyo kuwafanya kuwa wazalishaji mali. Vile vile, tafiti zinaonesha kuwepo kwa uhusiano mkubwa kati ya michezo na uongozi. Ili timu iweze kufanikiwa ni lazima iwe na viongozi wazuri watakaowezesha wachezaji kushindana kwa mbinu na maarifa zaidi kuliko timu pinzani. Hivyo, kwa kushiriki michezo tunakuza mbinu zetu za uongozi (Leadership skills). Aidha, ili kushinda ni lazima wachezaji wacheze kwa umoja,ushirikiano na kwa kutumia mbinu za pamoja. Hivyo, kwa kushiriki michezo tunajenga tabia ya kufanya kazi kwa bidii na kwa umoja (Teamwork). Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge na Ndugu Wanamichezo; Nimefahamishwa kuwa tamasha hili limepangwa kufanyika mara nne kwa mwaka, na hii ni mara ya pili kufanyika kwa mwaka huu. Kwa mantiki hiyo, ningependa kuchagiza kuwa tamasha hili litumike pia kama sehemu ya maandalizi ya ushiriki wa Bunge letu kwenye Mashindano ya michezo ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mbali ya kuimarisha udugu na umoja baina ya Mabunge yetu, ningependa kuona Bunge letu linaibuka na ushindi katika mashindano hayo. Aidha, tamasha hili limekuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2020 ambayo katika katika Sehemu ya 242 inaeleza umuhimu wa sekta ya michezo katika kutoa burudani, kuimarisha afya na kuunganisha jamii. Kadhalika, Sehemu ya 243 (c) ya Ilani ya Uchaguzi imejielekeza katika kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi na kuanzisha vilabu vya michezo na matamasha ya mazoezi ili kuboresha afya zao na kujikinga na magonjwa yasiyoambukizwa. Nawapongeza kwa kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge na Ndugu Wanamichezo; Napenda nihitimishe hotuba yangu kwa kuwapa changamoto ya tafakari kama ifuatavyo:-Kwanza, Bunge lifikirie kufanya semina/mjadala utakaolenga kuibua mapendekezo na mikakati mipya ikiwemo aina za uwekezaji endelevu, kutambua na kulea vipaji n.k. vitakavyowezesha michezo ambayo Tanzania inaipa kipaumbele (Tanzania ina competitive advantage) ili kushinda katika mashindano ya kikanda na kimataifa katika kipindi kifupi kwenda mbele. Pili, napenda kuwahimiza Wabunge wa kila mkoa kwa umoja wao au mmoja mmoja kuwa mstari wa mbele kuhamasisha na kulea timu za michezo katika mikoa/majimbo hususan timu za wanawake, vijana wa shule za msingi na sekondari na watu wenye ulemavu. NB: Wabunge kutoka Mkoa wa Kigoma anzeni na timu yetu ya Mashujaa ili itoke kidedea huko Mbeya leo!! Tatu, kwa kupitia tukio hili, si kwamba Bunge limetoa hamasa tu bali elimu kwa watanzania juu ya kutunza afya, kuwepo kwa magonjwa yasiyoambukizwa, jinsi ya kuyatambua na kujikinga pale inapowezekana. Rai yangu kwenu, hata baada ya tamasha hili, ni kuendelea kuhimiza watanzania wote kuishi maisha yanayofuata misingi ya afya bora na kuendelea kufanya mazoezi. Aidha, napenda kuwasihi Watanzania wenzangu, kuufanya utaratibu wa kufanya mazoezi kuwa ni wa kudumu kwa kila mmoja ili kujiepusha na maradhi na pia kujipunguzia sisi wenyewe na kuipunguzia Serikali mzigo mkubwa wa gharama za matibabu ya magonjwa yanayoweza kuepukika kwa kufanya mazoezi mara kwa mara. Nne, uwepo wa miundombinu stahiki ni muhimu katika kukuza michezo na kuchochea mwamko wa kushiriki michezo miongoni mwa wananchi. Hivi sasa, miundombinu ya michezo ni michache na maeneo mengi yaliyotengwa kwa ajili ya michezo yamebadilishiwa matumizi na kuyageuza kuwa makazi ama maeneo ya biashara. Tushirikiane kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya michezo yanalindwa na hayabadilishiwi matumizi. Vile vile, ulinzi wa maeneo ya michezo uendane na uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti kuzunguka viwanja vya michezo ili kuhakikisha upatikanaji wa hewa safi wakati wananchi wanapofanya mazoezi au kushiriki mashindano mbalimbali. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge mliopo, Ndugu Washiriki; Napenda nihitimishe hotuba yangu kwa kuwapongeza nyote kwa mara nyingine tena kwa mwamko na ushiriki wenu mzuri katika tamasha hili. Nampongeza pia Mheshimiwa Spika na Waandaaji wote wa tamasha kwa maandalizi mazuri na ningependa kuona matamasha haya yanaendelea kufanyika kama ilivyopangwa ili kufikia malengo. Baada ya kusema hayo, sasa natamka kuwa Tamasha hili la michezo limefunguliwa rasmi. Mungu Ibariki Tanzania. Asanteni sana kwa kunisikiliza na nawatakia tamasha jema.