Mkurugenzi wa Uamuzi (CMA) Mhe. Vallensi Wambali leo Juni 26, 2023 Jijini Dodoma akiwa katika kipindi cha Televisheni cha Dodoma cha “The Morning Power” anaelezea kuhusu mfumo wa zamani ulivyokuwa unatumika katika kutatua migogoro hadi kupelekea kuanzishwa kwa mfumo mpya wa utatuzi wa migogoro ya kikazi kwa njia ya mtandao.
Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imeandaa Mfumo wa kielektroniki wa utatuzi wa migogoro ya kikazi ambao utasaidia usikilizaji wa mashauri kufanyika kwa njia ya mtandao.
Amesema hayo, Mkurugenzi wa Uamuzi Bw. Vallensi Wambali leo Juni 26, 2023 wakati akishiriki katika kipindi cha “The Morning Power” kilichoratibiwa na televisheni ya Dodoma (Dodoma Tv), jijini Dodoma.
Aidha, amesema kuwa Taasisi hiyo ina jukumu la kuhakikisha masuala ya utatuzi wa migogoro ya kikazi kwa njia ya Usuluhishi na Uamuzi yanafanyika kwa ufasaha hivyo, mfumo huo mpya utarahisisha utekelezaji wa shughuli hizo.
Kwa upande mwingine, Bw. Wambali amesema ifikapo mwezi Julai 2023 mfumo huo utakuwa umesajiliwa na kuanza kufanya kazi rasmi na lengo ni upatikanaji wa maendeleo kwa haraka kwa kusikiliza mashauri haraka na kupunguza taratibu zilizokuwepo awali kwa njia ya makaratasi.
“Dhamira ya Serikali yetu ni kuboresha na kuendeleza miundombinu na mifumo ya TEHAMA na katika maadhimisho ya wiki ya Sheria mwaka huu 2023, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alisisitiza swala la utatuzi wa mashauri kuanza kufanyika kwa njia ya mtandao ili wananchi wapate huduma kwa urahisi na haraka” amesema.