Mamlaka za Halmashauri za Wilaya nchini na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), zimetakiwa kufanya kazi kwa kushirikiana na kuweka mazingira bora ya utoaji wa huduma za Leseni za Biashara nchini.
Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Mhe. Juma Chikoka ametoa wito huo leo tarehe 26 Juni, 2023 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya Maafisa Biashara kutoka katika mikoa 10 ya Tanzania Bara, yanayofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mjini Musoma.
“Kwakuwa Sheria ya Leseni za Biashara inasimamiwa na kutekelezwa na Mamlaka hizi mbili yaani BRELA na Halmashauri, kuna umuhimu wa Mamlaka hizi mbili kufanya kazi kwa ukaribu na kwa kuelewana na kushauriana njia bora za kuboresha utoaji wa huduma za Leseni na kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wafanyabiashara wetu na hivyo kuongeza wigo wa walipa kodi, kuongezeka kwa ajira na ukuaji wa uchumi wa nchi kwa ujumla wake”, amesema Mhe.Chikoka.
Pia, amewataka Maafisa Biashara hao kupitia mafunzo yanayotolewa na BRELA kuwa chachu ya kuwawezesha kufanya kazi zao kwa weledi na ufanisi katika kutoa huduma kwa wafanyabiashara nchini.
Ameongeza kuwa, jukumu mojawapo la kisheria la BRELA ni utoaji wa Leseni za Biashara kundi “A” kama ilivyo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs) Tanzania Bara, ambazo kwa kupitia Sheria hiyo hiyo ya Leseni za Biashara zinatoa Leseni za Biashara kundi “B”, hivyo ni muhimu kufanya kazi kwa ukaribu.
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, Mkuu wa Sehemu ya Leseni za Biashara, Bw. Tawi Kilumile ameeleza kuwa, ni matarajio ya BRELA kwamba Maafisa Biashara watakuwa Mabalozi wazuri kwa maafisa wengine.
BRELA imeendelea kuratibu na kufanya mafunzo haya ya kuwajengea uwezo Maafisa Biashara wa Mikoa na Halmashauri zote ili waweze kuielewa kiundani Sheria ya Leseni za Biashara (Sura 208) na Sheria ya Taifa ya Usajili na Utoaji wa Leseni za Viwanda (Sura 46).
“Hivyo, kupitia mafunzo haya tunaimani kuwa maafisa biashara mtakwenda kuwa mabalozi wazuri wa BRELA na Serikali kwa ujumla na kuwa mfano bora kwa Maafisa wengine katika utoaji wa huduma bora na wezeshi”, ameeleza Bw. Kilumile.
Mafunzo haya yaliyoratibiwa na BRELA yanahudhuriwa na Maafisa Biashara kutoka Mikoa ya Mara, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Tabora, Kigoma, Arusha, Manyara na Kilimanjaro.