Home LOCAL WATUHUMIWA SITA KIZIMBANI WAKIDAIWA KUMUUA MILEMBE.

WATUHUMIWA SITA KIZIMBANI WAKIDAIWA KUMUUA MILEMBE.

Watu sita wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Geita Mkoani Geita wakishtakiwa kwa kosa la kumuua aliyekuwa mfanyakazi wa kampuni ya madini ya dhahabu (GGML) Milembe Seleman mwenye umri wa miaka (43).

Watuhumiwa hao waliopandishwa mahakamani katika kesi namba 12/2023 ni pamoja na Dayfath Maunga(30), Safari Labingo(54), Genja Lubingo(30), Musa Lubingo (33), Maige Fundikira (37) na Ceslia Macheni (55).

Mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Johari Kijuwile, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Scolla Teffe ameieleza Mahakama hiyo kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa la mauji kinyume na kifungu cha 196 & 197 cha kanuni ya adhabu .

Amedai Aprili 26, 2023 Dayfath Maunga na wenzake watano huko katika maeneo ya Mwatulole halmashauri ya Mji wa Geita wakishirikiana kwa pamoja walimuua Milembe Seleman na Washtakiwa hao hawakupaswa kuzungumza chochote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji.

Ikumbukwe kuwa Milembe Seleman (43) aliyekuwa mfanyakazi wa kitengo cha Ugavi katika kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu (GGML) aliuawa Aprili 26, 2023 kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo kichwani, usoni na mikononi ambapo kiganja kimoja cha mkono kiliondolewa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 7, 2023 itakapotajwa na washtakiwa wote wamerudishwa mahabusu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here