Home BUSINESS NORWAY NA SUA KUDUMISHA USHIRIKIANO

NORWAY NA SUA KUDUMISHA USHIRIKIANO

NA: FARIDA MANGUBE, MOROGORO.

Serikali ya Norway imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania kupitia Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo ( SUA ) katika miradi mbalimbali ikiwemo kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yameelezwa mjini Morogoro na Mhe. Balozi wa Norway Tanzania, Elisabeth Jacobsen alipotembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na kuona mambo mbalimbali ikiwemo namna ya Chuo hicho kinavyofanya miradi ya ushiriki wa vijana kwenye kilimo sambamba na upanuzi wa ajira kwa vijana hao.

Amesema Tanzania na Norway zimekuwa na ushirikiano mzuri kwa zaidi ya miaka 50 hivyo malengo yao ni kuendeleza ushirikiano huo kwa kuanzisha na kuendeleza miradi ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ya hewa ukaa.

“Tutaongea na Makamu Mkuu wa Chuo namna ya kushirikisha Chuo hiki na vyuo vya Norway pia kuna mambo mengi ya kushirikiana lakini hatutashiriki kwenye kilimo pekee bali hata kwenye masuala ya miradi ya mabadiliko ya hali ya hewa .” Alisema Mhe. Balozi Elisabeth

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda amesema ujio wa Balozi huyu chuoni hapo ni sehemu ya kudumisha ushirikiano uliopo baini yao.

“Norway ndiyo iliyotusaidia kuanzisha Ndaki ya Misitu, Ndaki ya Uzalishaji wa Wanyama vilevile hivi karibuni wametusaidia kuanzisha kituo cha hewa ukaa katika miaka 50 iliyopita kwa nyakati tofauti walitusaidia kugharamia miradi mbalimbali ya tafiti, ambapo kupitia tafiti hizo Chuo chetu kimeweza kukua.” Alisema Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Chibunda.

Ameongezea kwa kusema, ujio wa Balozi huyo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuvitaka vyuo vyote vikuu nchini visiwe vyuo vikuu vya watu wa ndani bali vifanyiwe umataifishaji (kuwa na wanafunzi na walimu wa kimataifa) hivyo SUA imekuwa ikifikia Balozi mbalimbali na kuwajengea uelewa kuhusu mambo yaliyopo chuoni hapo.

Naye mmoja wa wahitimu wa SUA ambaye kwa sasa ni mkulima katika Kituo Atamizi kilichopo chuoni hapo Happiness Nyanga amesema atatumia maarifa na ujuzi alioupata chuoni hapo katika kutimiza malengo yake ya kuwa mkulima mkubwa wa mazao ya mboga na matunda.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here