Dkt. Mshangila akiwa kwenye chumba cha upasuaji kwenye hospitali ya wilaya ya Mbarali ambapo kambi ya upasuaji wa mtoto wa jicho inayofadhiliwa na Hellen Keller International.
Huduma za upasuaji wa kuondoa mtoto wa jicho zikiendelea kwenye ‘theater’ ya hospitali ya wilaya ya Mbarali.Kambi hiyo inafanyika kwa ufadhili wa Shirika la Hellen Keller International kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.
Daktari bingwa wa macho kutoka hospitali ya rufaa ya kanda-Mbeya Dkt Barnabas Mshangila akiwakagua wagonjwa wa mtoto wa jicho waliofanyiwa upasuaji mara baada ya kuondolewa. bandeji.
Bibi Victoria Mronji mkazi wa kijiji cha Muungano ambaye alikua na shahuku kubwa ya upasuaji akisaidiwa kutoa nje ya wodi ili kuondolewa bandeji.
Kundi la pili la Wakazi wa Halmashauri ya Mbarali waliofanyiwa upasuaji wa kuondoa mtoto wa jicho wakisubiri kuondolewa bandeji.Â
Na: WAF-Mbarali
Wazazi wametakiwa kuwapeleka watoto wenye matatizo ya mtoto wa jicho wanayozaliwa nayo au yaliyotokana na majeraha ili kupata matibabu sahihi na kumuwezesha ubongo kukua vizuri na kuona vizuri.
Rai hiyo imetolewa leo na Daktari Bingwa wa Macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) Dkt. Barnabas Mshangila kwenye kambi ya upasuaji wa mtoto wa jicho inayoendelea katika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali ambayo inaratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Hellen Killer International la hapa nchini.
Dkt. Mshangila amesema kawaida mtoto anapokua anatakiwa macho yake yaone vizuri ili ubongo na wenyewe uweze kukua hivyo mtoto anapoumia akiwa chini ya miaka (7) na asipopelekwa hospitali kufanyiwa upasuaji husababisha kutokuona vizuri ukubwani.
“Mtoto asipofanyiwa matibabu kwa wakati na anapofanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho akiwa mtu mzima, jicho huwa halioni vizuri kwani mwanga unakuwa haujaingia wa kutosha na kufanya ubongo nao usikue, ushauri wangu ni vyema wazazi kuwapeleka kwenye vituo vya afya watoto kwa ajili ya uchunguzi pale mtoto anapopata majeraha kwani anaweweza asisikie maumivu”. Amesema Dkt. Mshangila.
Kwa upande wa waliofanyiwa upasuaji Dkt. Mshangila amesema ni vyema wakafuata masharti wanayopatiwa ikiwemo kutokufanya kazi ngumu na kutokukaa sehemu yenye moshi pamoja na vumbi pia kuhudhuria kliniki na kuonana na wataalamu kwa tarehe walizopangiwa.
Aidha, amesema mtu aliyefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho tatizo hilo haliwezi kujirudia mara baada ya upasuaji ila wapo baadhi ya watu huwa inaweka ukungu kwenye sehemu ambayo inaachwa wakati wanaweka lenzi ya mwanzo.
“Kuna wachache inaweka ukungu kwa kuona jicho linafifia tena lakini inakua sio kama mtoto wa jicho la mwanzo na huwa labda baada ya miaka mitatu, akija hospitali upasuaji wake huwa sio mkubwa na hurudi kuona tena”. Amesema.
Hata hivyo amewatoa hofu baada ya watu ambao wana matatizo ya mtoto wa jicho ambao hudhani akifanyiwa upasuaji hawawezi kuona tena na kuwasihi kujitokeza kwa wingi ili kuweza kupatiwa huduma hizo ambazo zimesogezwa karibu na makazi yao.
Dkt. Mshangila ameongeza kuwa yapo matatizo mengine yanayosababisha upofu ambao hautibiki hivyo kama wataalamu kabla ya upasuaji wa mtoto wa jicho huwafanyia uchunguzi kama kuna shida nyingine kama presha ya macho, huwashauri wajue endapo watafanyiwa upasuaji hawatoona vizuri.
Mtoto wa jicho ni tatizo linalosababisha ukungu kwenye kioo (lenzi) ambapo mboni ya jicho hubadilika na kuwa jeupe na hivyo upasuaji hufanyika ili kutoa lenzi yenye ukungu na kuweka lenzi isiyo na ukungu na visababishi vyake ni mabadiliko ya mwili yanayoambatana na umri.