Home BUSINESS WAHARIRI WASISITIZA KULINDWA KWA MIRADI YA MAENDELEO

WAHARIRI WASISITIZA KULINDWA KWA MIRADI YA MAENDELEO

NA: FARIDA MANGUBE, MOROGORO.

Jukwaa la wahariri Tanzania (TEF) limetembelea kiwanda cha kuchakata nyama cha Nguru Hill kinachomilikiwa na mfuko wa pensheni kwa watumishi wa umma (PSSSF) na wabia wengine kilichopo Mvomero mkoani Morogoro.

Uwepo wa kiwanda hicho umeleta mapinduzi makubwa ya katika sekta ya ufugaji na kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji mkoani Morogoro kwani kitasaidia kupunguza muingiliano wa jamii hizo mbili.

Wakizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda hicho chenye uwezo wa kuchinja Ng’ombe 100 na Mbuzi 1000 kwa wakati mmoja, wahariri hao wameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi imara wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa inayofanya katika kuwekeza katika sekta ya viwanda hapa nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti waJukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile amesema kwa nchi zilizoendelea mifuko ya ya Hifadhi ya Jamii imekuwa chazo kikubwa cha kukuza mitaji ya watu hivyo uwekezaji uliofanywa na PSSSF umeonyesha ukomavu wa mfuko huo katika kukuza uchumi wa watu.

“Niwaombe PSSSF wahakikishe mradi huu wanaulinda na miradi mingine, leo tulivyofika tukaona hatua za kuchinja na huduma za kisasa, si vyema sana baada ya miaka kadhaa mbele tukapita hapa tuambiwe kilikuwepo kiwanda kisa wafanyakazi hawakutimiza wajibu wao vinzuri”. amesema Balile.

Aidha amesema kuna haja ya kuitunza miradi mbalimbali inayoanzishwa na Serikali kupitia mashirika ya umma na mifuko ya jamii kwani imekuwa chachu ya kukuza uchumi wa vijana na Taifa kwa ujumla.

Naye meneja uhusiano na elimu kwa umma PSSSF James Mlolwa amesema PSSSF imewekeza Dola za Kimarekani 3,900.000 kwa kushirikiana na wadau wengine katika kufufua kiwanda hicho ambacho kwa sasa kimeanza kufanya kazi.

Aidha amewahakikishia watanzania kuwa uwekezaji huo umeleta manufaa makubwa kwa Taifa, kwani umeweza kutoa ajira kwa vijana pamoja na kuwepo kwa uhakika wa soko la Ng’ombe na Mbuzi kwa Mkoa wa Morogoro na mikoa ya  jirani.

Kiwanda hicho cha Nguru Hill kinamilikiwa na PSSSF kwa kushirikiana na wawekezaji wenza kampuni ya Eclipse Investiment LLC kutoka nchini Omani pamoja na Kampuni ya Busara Investiment LLP.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here