Home BUSINESS TANI MILIONI 20 ZA SHEHENA MCHANGANYIKO KUHUDUMIWA KATIKA BANDARI YA DAR ES...

TANI MILIONI 20 ZA SHEHENA MCHANGANYIKO KUHUDUMIWA KATIKA BANDARI YA DAR ES SALAAM.

Bandari ya Dar es salaam inakusudia kuhudumia Tani Milioni-20 za Shehena mchanganyiko kwa mwaka, kufuatia maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. Samia Suluhu Hasaan.

Tangu Rais Dkt. Samia aingie madarakani, ameshatoa zaidi ya shilingi Bilioni-573 ili kuwekeza katika Bandari ya Dar es salaam ikiwemo ununuzi wa mitambo ya kisasa ya kupakia na kushusha Makontena.

Lengo la uwekezaji huo ni kuchochea kasi na ukuaji uchumi, ambapo takwimu zinaonesha zaidi ya asilimia 40 ya mapato yatokanayo na kodi yanatoka katika Bandari.

Mkurugenzi Mkuu wa Bandari ya Dar es salaam, Mrisho Suleiman Mrisho, ametangaza mafanikio hayo wakati akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa kituo cha utangazaji cha Uhuru FM waliotembelea kujionea maboresho ya Bandari hiyo ya Dar es salaam.

Kwa mujibu wa Mrisho, uduni wa miundombinu katika Bandari hiyo ilikuwa ni kikwazo bandarini, hivyo, wamemshukuru Rais Samia kwa uwekezaji huo mkubwa.

Aidha, Bandari ya Dar es salaam, hivi sasa ina uwezo wa kuhudumia meli ya ukubwa wa aina yoyote na kwa wakati wowote, hii ikitokana na maboresho yaliyofanyika ikiwemo ujenzi wa Gati mpya namba 0 yenye uwezo wa kuegesha shehena ya magari zaidi ya 6000 kwa wakati mmoja.

Chini ya maboresho hayo, Bandari ya Dar es salaam imekuwa ikihudumia pia mteja mpya ambaye ni nchi ya Zimbambwe, ambapo bidhaa kubwa ya nchi hiyo inayopita katika Bandari hiyo ni magari.

Kuhusu hali ya Ulinzi, Mkurugenzi Mkuu wa Bandari ya Dar es salaam, Mrisho, amesema hali ya ulinzi katika Bandari ya Dar es salaam imeimarishwa zaidi, hivyo hakuna wizi wa mafuta wala mizigo kama inavyodaiwa na wananchi wakati unaposhuka kupitia Bandari hiyo.

Amesema maeneo yote ya Bandari yamefungwa Kamera za kisasa zaidi ya Mia Nne Sabini, sambamba na uwepo vyombo vya ulinzi, hivyo kuifanya Bandari hiyo kuwa salama wakati wote.

Kuhusu madai ya uchache wa Meli, Mkurugenzi Mkuu wa Bandari ya Dar es salaam, Mrisho amesisitiza kuwa zaidi ya Meli kubwa 50 zimehudumiwa kwa siku 17 za mwezi huu wa Nne katika Bandari, huku malengo yao yakiwa ni kuhudumia Meli 100 hadi kufikia mwisho wa mwezi huu.

Ufafanuzi huo wa Mrisho, umaekuja kufuatia baadhi ya watu kudai kuwa kumekuwa na idadi ndogo ya meli zinazotia Nanga katika Bandari hiyo ya Dar es salaam.

“Jamani nakanusha sio kweli Meli zinazopita katika Bandari ya Dar es salaam zimepungua kama inavyodaiwa, ukweli ni kwamba katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa sana la meli zinazotia Nanga Bandarini ikiwemo meli kubwa ya Watalii zaidi ya 400 kutoka Marekani” amesema Mrisho.
Kwa upande wake,

Naibu Mkurugenzi wa Uhuru FM, Amina Aziz, amesema kujionea shughuli zinazofanywa na Bandari ya Dar es salaam kumetoa fursa ya kuona namna Serikali ilivyowekeza na kutoa nafasi ya kuwaelimisha wananchi kuhusu Bandari hiyo inavyofanya kazi na mafanikio yake.

Wafanyakazi wa Uhuru FM wamefanya ziara katika Bandari ya Dar es salaam lengo likiwa ni kujionea Bandari inavyofanya kazi na mafanikio yake baada ya serikali kutoa fedha za kuboresha Bandari hiyo.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here