Home BUSINESS SERIKALI KUHAKIKI UPYA MAOMBI YA KIFUTA JASHO NA KIFUTA MACHOZI KWA WANANCHI...

SERIKALI KUHAKIKI UPYA MAOMBI YA KIFUTA JASHO NA KIFUTA MACHOZI KWA WANANCHI WA WILAYA YA NANYUMBU

Serikali imesema itahakiki upya maombi ya kifuta jasho na kifuta machozi kwa Wananchi walioathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu katika Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu ili kuwapatia stahili zao

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nanyumbu, Mhe. Ally Yahya Mhata aliyetaka kujua idadi ya Wananchi wa Jimbo la Nanyumbu ambao wamefidiwa kutokana na uharibifu uliofanywa na tembo katika mashamba yao.

“Nimuombe Mheshimiwa Mbunge kwenye hili suala la takwimu nitazichukua kutoka kwake lakini pia tutaenda kuhakiki upya katika maeneo hayo ili wananchi waweze kulipwa stahili zao” Mhe. Masanja amesisitiza.

Awali, Mhe. Masanja alifafanua kuwa mnamo tarehe 21 Machi, 2023 Wizara ilifanya malipo ya kifuta jasho ya kiasi cha shilingi milioni 5.1 kwa wananchi saba (7) wa vijiji vya Michenjeuka, Lukula, Masuguru na Mpombe walioharibiwa mazao.

Aidha, Mhe. Masanja amesema mwezi Machi mwaka huu Wizara ilipokea maombi mapya 12 ya wananchi wa vijiji vya Nanyumbu na Marumba ambayo yanaendelea kushughulikiwa kwa ajili ya kuandaa malipo.

Ili kuondokana na migongano baina ya binadamu na wanyamapori, Mhe. Masanja amewaasa wananchi kuacha kuendelea kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo ya shoroba za wanyamapori.

Akijibu swali la Naibu Spika, Mhe. Mussa Zungu kuhusu kero ya popo katika Kata ya Kivukoni Jimbo la Ilala, Mhe. Masanja amesema Serikali imeshaanza kuifanyia kazi changamoto hiyo kupitia Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania(TAWIRI) ambayo imeshaanza kutafuta mbinu mbadala kuhakikisha popo hao wanaondoka kabisa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here