Home BUSINESS NCT NA DMI WAINGIA MAKUBALIANO YA KUTOA MAFUNZO KWA MABAHARIA

NCT NA DMI WAINGIA MAKUBALIANO YA KUTOA MAFUNZO KWA MABAHARIA

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dkt. Florian Mtey (kulia aliyekaa) na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Dkt. Tumaini Gurumo  (kushoto aliyekaa) wakitia saini nyaraka za makubaliano (MoU) ya kutoa mafunzo kwa Mabaharia katika fani mbalimbali ikiwemo upishi. Hafla hiyo imefanyika leo April 19, 2023 katika Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Jijini Dar es Salaam.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dkt. Florian Mtey (kulia) na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Dkt. Tumaini Gurumo  (kushoto)  wakikabidhiana nyaraka mara baada ya kutia saini makubaliano (MoU) ya Mashirikiano ya kutoa mafunzo kwa Mabaharia katika fani mbalimbali ikiwemo upishi.

 

Baadhi ya Maafisa wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), na Watumishi wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) wakipiga makofi kupongeza hatua hiyo ya makubaliano ya Taasisi hizo.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dkt. Florian Mtey (kulia) akizungumza na Wajumbe kutoka DMI na NCT, pamoja na waadhishi wa habari muda mfupi kabla ya kusaini nyaraka za makubaliano hayo.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Dkt. Tumaini Gurumo  (kushoto) akizungumza alipokuwa akitoa hotuba yake muda mfupi kabla ya kutiliana saini Makubaliano hayo.

(PICHA NA: HUGHES DUGILO)

Na:Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM

Katika kuhakikisha vijana wa kitanzania wanapata fursa za ajira katika maeneo mbalimbali yakiwemo katika meli za kitalii, Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), pamoja na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) wameingia makubaliano ya kushirikiana kutoa mafunzo kwa Mabaharia katika fani mbalimbali ikiwemo upishi zitakazo wawezesha kufanya kazi katika meli za Kitalii.

Mafunzo hayo yanayotarajiwa kuanza hivi karibuni yatawapa uwezo wahitimu wa fani ya upishi Melini kupata Cheti cha fani hiyo kitakacho muwezesha kupata kazi katika Meli za kitalii mahali popote Duniani.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubalino hayo iliyofanyika leo april 19,2023 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dkt. Florian Mtey amesema kuwa hatua hiyo ya mashirikiano kati ya Taasisi hizo mbili kutafungua milango kwa Mabaharia wapishi kufanyakazi zao Kwa weledi na ufanisi.

“Kupitia Mashikiano haya, vijana wa Kitanzania wanapata fursa za ajira katika meli za Kitalii zinazosafirisha watalii Duniani, Chuo chetu cha Taifa cha Utalii pamoja na Chuo cha Bahari cha Dar es salaam, tunaingia makubaliano ya kushirikiana kutoa mafunzo kwa mabaharia katika fani ya Upishi na vilevile tutaongeza wigo wa mafunzo katika fani nyingine za ukarimu kwenye meli  yatakayowezesha  vijana  kufanya kazi  kwa weledi na ufanisi.”

“Wapishi wa Melini kama Mabaharia lazima wawe wamefunzwa vyema na kuhitimu ili waweze kupika na kuhudumia kwa kiasi na kwa kiwango cha ubora unaohitajika katika chakula chenye lishe bora ambacho kinakidhi mahitaji ya Kitamaduni, Kidini, pamoja na uhifadhi wa chakula kwa usafi” amesema Dkt. Mtey.

Amesema kuwa mashirikiano hayo ni wazi kuwa yatakwenda kuleta tija na kuboresha huduma zitolewazo katika meli za kitalii na kutimiza malengo ya Serikali ya kuongeza idadi ya watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025 nchini Tanzania.

Aidha Dkt. Mtey amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake mbalimbali za kuhakikisha Utalii unaimarika nchini ikiwemo uzinduzi wa Filamu ya ‘Tanzania: The Royal Tour’ ambayo imesaidia kuitangaza Tanzania na vivutio vyake kwa ujumla na kupelekea kuleta hamasa kwa watalii kutembelea.

“Tumeshuhudia meli nyingi za Kitalii zikitia nanga katika Ardhi ya Tanzania” Hivyo kama Chuo cha Utalii na Chuo cha Bahari cha Dar es salaam tunaunga jitihada hizo kwa kuzalisha vijana watakao fanyakazi kwenye meli” amesema Dkt. Mtey.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Dkt. Tumaini Gurumo amesema kuwa Mkataba huo utapelekea  taasisi hizo mbili kufikia malengo ya kuisadia Serikali kwa kuongeza tija ya ajira kwa vijana wenye fani ya Ubaharia na kuleta tija zaidi katika uchumi wa Bluu.

“Tunasikia Uchumi wa Bluu ukipewa kipaumbele, lakini pia tunasikia habari ya ajira kwa vijana imekuwa ikizungumzwa mara, kwa mara, fursa hizi tunaziendeleza kwa kuwawezesha vijana kuzifikia ili waweze kujikwamua kiuchumi.

“Lengo na mikakati yetu ni kusaidia juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha kunakuwepo na fursa za ajira kwa vijana” amesema Dkt. Gurumo.

Akizungumzia Majukumu ya Chuo hicho katika kutoa Elimu na Mafunzo, Dkt. Gurumo amesema Chuo cha DMI kimekuwa kikitoa mafunzo kwa Manahodha na Wahandisi pekee lakini baada ya kuona  kuna muelekeo mkubwa wa ukuaji wa Sekta ya Utalii wa Majini hasa kwenye uchumi wa Bluu ndipo wakabaini fursa nyingine nyingi katika kada saidizi za Mabaharia.

“tunapozungumzia watumishi wa Melini tunakuwa na maeneo matatu muhimu, eneo la kwanza ni Manahodha, Wahandisi na kada saidizi, sasa hizi kada saidizi ndio tumekuwa hatuzifanyii kazi.

“Baada ya kuona kwamba kuna muelekeo mkubwa sana wa ukuaji wa Sekta ya Utalii wa majini ndipo tulipoanza kutazama ni jinsi gani tunaweza kuwapata watanzania ambao watakuwa na sifa na vigezo vya kimataifa vitakavyowasaidia kufanyakazi katika hizi meli za kitalii ili waweze kujiongezea kipato kwa sababu nafasi za ajira ziko nyingi” ameongeza Dkt. Gurumo.

Baadhi ya watumishi wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) katika hafla hiyo.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dkt. Florian Mtey (wa nne kulia) na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Dkt. Tumaini Gurumo  (wa tatu kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Baadhi ya Maafisa wa Taasisi hizo mbili mara baada ya kumalizika kwa hafla hiyo iliyofanyika leo April 19,2023 Jijini Dar es Salaam.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dkt. Florian Mtey (kulia) na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Dkt. Tumaini Gurumo  (kushoto) wakiwa katika mazungumzo mafupi kabla ya kuagana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here