Home LOCAL KANISA ANGLIKANA TANZANIA LAUNGANA NA DINI NYINGINE KUMUAGA ASKOFU KASAGARA LAKE RUKWA...

KANISA ANGLIKANA TANZANIA LAUNGANA NA DINI NYINGINE KUMUAGA ASKOFU KASAGARA LAKE RUKWA MPANDA

Na: Maiko Luoga Mpanda

Waumini wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Lake Rukwa machi 26, 2023 walishiriki Misa ya shukrani ya kumaliza salama muda wa utumishi wa Askofu wa kwanza wa Dayosisi hiyo Mathayo Kasagara iliyofanyika katika Kanisa Kuu Anglikana Kristo Mfalme Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.

Misa hiyo iliongozwa na Muhashamu Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania na Dayosisi ya Tanga Maimbo Mndolwa ambae alisema Askofu Kasagara amefanya kazi njema ya injili tangu Dayosisi hiyo ilipoanzishwa mwaka 2010 hadi sasa 2023 anapomaliza muda wake wa utumishi ndani ya Kanisa.

“Tunamwambia Mungu asante kwa zawadi ya Baba Askofu Kasagara na ushahidi wa kazi njema ni Kanisa hili tunapoabudu leo, Mungu atukuzwe kwa kumtunza Baba Askofu, Familia yake na Dayosisi hii, tutumie nafasi hii pia kuwaonya wote watakaofanya Kampeni na kutoa rushwa kutafuta nafasi ya Askofu wa Dayosisi ya Lake Rukwa Kanisa ombeni Mungu awainulie mtu wake” alisema Askofu Mndolwa.

Akisoma hati ya kupokea mamlaka ya Askofu wa Dayosisi ya Lake Rukwa Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Canon Bethuel Mlula alisema, Dayosisi hiyo itakuwa chini ya uangalizi wa Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania hadi hapo Askofu mwingine atakapopatikana kisha ikafuata hatua ya Askofu Kasagara kukabidhi fimbo ya mamlaka ya Kiaskofu kwa Askofu Mkuu.

Awali akitoa hotuba kwa washiriki wa Misa hiyo Askofu Dickson Chilongani wa Dayosisi ya Central Tanganyika, Makamu wa Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania (DEAN) alimtaka Askofu Kasagara kama wapo waliomtesa wakati wa utumishi wake kusamehe na kuachilia kwakuwa ni kazi aliyoagizwa na Mungu.

“Baba Askofu Kasagara kazi uliyoitiwa ilikuwa njema na ngumu katika hali ya kibinadamu, kama wapo waliokutesa na kukuumiza nakusihi samehe na kuachilia ili utumishi wako uwe mwema mbele za Mungu” alisema Askofu Chilongani.

Akizungumza wakati wa kuwaaga Waumini wa Dayosisi ya Lake Rukwa Askofu Mathayo Kasagala alitumia Madhabahu ya Kanisa Kuu la Dayosisi hiyo kuomba msamaha wote aliowakwaza na kutoa neno la msamaha na Baraka kwa wale waliomkwaza wakati akitekeleza majukumu ya Kiaskofu.

“Nitumie nafasi hii kuomba radhi wote niliowakwaza wakati wa utumishi wangu nami naachilia msamaha na Baraka kwa wote walionikwaza ndio maana leo nimewashirikisha watu wote mwili na damu ya Yesu hapa, tukumbuke baada ya hapa atakuja Askofu mwingine naomba tumpe ushirikiano kama mlivyonipa mimi ili kufanikisha kazi zilizopo mbele yetu”

Akizungumza kwa niaba ya Nyumba ya Maaskofu wa Kanisa Anglikana Tanzania Askofu Elias Chakupewa wa Dayosisi ya Tabora alisema Nyumba hiyo ilikuwa ikijumuisha uwepo wa Askofu Kasagara ambae alikuwa na mchango wa maendeleo katika kulijenga Kanisa hivyo katika kipindi hiki wanamtakia mapumziko mema.

Baadhi ya waumini walioshiriki Ibada hiyo kutoka maeneo tofauti ya Dayosisi ya Lake Rukwa ikiwemo Sumbawanga na Mpanda walisema, wanaamini Askofu Kasagara hajamaliza kazi ya Mungu kwakuwa bado nasaha na maoni yake yataendelea kuhitajika katika kujenga injili na Kanisa la Mungu huku wakimpongeza kwa ujenzi wa Kanisa Kuu la Kisasa Mpanda mjini.

Misa hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa Kanisa Anglikana Tanzania, madhehebu mbalimbali akiwemo Shekh wa dini ya Kiislam Mkoa wa Katavi, viongozi wa Serikali na wadau ambao walikuwa wakishirikiana na Askofu Kasagara wakati wa utumishi wake.

Dayosisi ya Lake Rukwa inajumuisha sehemu ya utawala wa mikoa miwili ya Rukwa na Katavi ilianzishwa mwaka 2010 ikizaliwa kutoka Dayosisi ya Western Tanganyika yenye makao yake wilayani Kasulu mkoani Kigoma na Askofu Mathayo Kasagara aliwekwa wakfu kuwa Askofu wa kwanza wa Dayosisi hiyo mnamo Juni 2010 hadi kufikia mwaka 2023 Askofu Kasagara amehudumu kwa muda wa miaka 13.

Previous articleYASEMAVYO MAGAZETI LEO JUMATATU MACHI 27,2023
Next articleWAZIRI NAPE KUFUNGUA KONGAMANO LA 12 LA KITAALUMA LA JUKWAA LA WAHARIRI (TEF) MOROGORO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here