Wawakilishi wa michuano Kombe la Shirikisho Barani Afrika Yanga SC imefaniwa kukamata mamilioni ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuichapa timu ya TP Mazembe ya Congo kwa mabao 3-1 mchezo uliopigwa katika Dimba la Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Magoli ya Yanga yalipatikana katika dakika za mwanzoni mwa mchezo huo kupitia kwa mshambuliaji wake Kennedy Musonda katika dakika ya 7 ya mchezo huo akipiga kichwa kunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Juma Shabani, huku bao la pili likifungwa na Mudathir Yahaya katika dakika ya 11 ya mchezo huo goli lililodumu katika dakika zote za kipindi cha kwanza cha mchezo huo.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku timu zote mbili zikifanya mabadiliko ambapo TP Mazembe wakionekana kucharuka zaidi kwa kucheza kwa kasi na kufanikiwa kupata goli lililofungwa na Alex Ngonga kwa mpira wa adhabu uliomshinda mlinda mlango wa Yanga Didier Diara.
Timu ya Yanga ilipata bao lake la tatu katika dakika za lala salama za mchezo huo goli likifungwa na Twisila Kisinda kwa mkwaju mkali dakika ya 91 akipokea pasi ya Fiston Mayele aliyewaacha walinzi wa TP MAZEMBE.
Kufuatia ushindi huo timu ya Yanga inashika nafasi ya tatu katika kundi lao akiwa na alama 3, likiongozwa na US Monastir mwenye alama 4 na TP Mazembe wakiwa nafasi ya 2 wakiwa na alama 3 na mwisho ni AS Real de Bamako mwenye alama 1.
Michezo inayofuata katika Kundi hilo Yanga itaifuata RS de Bamako wakati TP MAZEMBE watawakaribisha US Monastir kutoka Tunisia.