TMDA
Home BUSINESS UMMY MWALIMU: UMEFIKA WAKATI KWA JAMII KUACHANA NA MATUMIZI YA KUNI NA...

UMMY MWALIMU: UMEFIKA WAKATI KWA JAMII KUACHANA NA MATUMIZI YA KUNI NA MKAA

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amesema umefika wakati kwa jamii ya Watanzania kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo ya gesi kama hatua mojawapo ya kukabikiana na mabadiliko ya tabianchi.Ameyasema hayo leo Februari 21,2023 wakati Kampuni ya Oryx Gas Tanzania ikigawa bure mitungi ya gesi 600 yakiwa na majiko yake kwa wanawake wajasiriamali wa Jiji la Tanga ambao wanatoka katika kata zote 27 huku thamani ya mitungi na majiko ikiwa Sh.milioni 51.

Waziri Ummy Mwalimu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa kuwepo kwa nishati mbadala ya kupikia hasa gesi ya Oryx inakwenda kusaidia kupunguza changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ya kukosekana kwa mvua za uhakika , ukame na athari nyingine za kiafya na kimazingira.

“Tunafahamu dunia inakabiliwa na janga la mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababisha athari nyingi kimazingira.Pia tunafahamu matumizi ya kuni na mkaa mbali ya kuharibu mazingira pia yanasababisha madhara ya kiafya kutokana na moshi.Hivyo majiko ya gesi ambayo yanakwenda kusaidia wana Tanga kuanza kujenga utamaduni wa kutumia nishati safi ya kupikia, hivyo kufanya mazingira kuwa salama.

Awali Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Araman Benoite amesema wamekabidhi mitungi ya gesi pamoja na majiko yake 600 kwa wanawake 600 kutoka vikundi mbalimbali vikiwemo vya wajasiriamali jijini Tanga ikiwa ni mkakati wao wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa yanayoharibu mazingira.

Benoite amesema kutokana na madhara ya gesi ya ukaa duniani, kampuni yao imekuwa mstari wa mbele kusaidia kuhamasisha matumizi ya gesi safi ya kupikia huku akieleza Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa yenye matumizi makubwa ya mkaa.

“Matumizi ya mkaa yana athari kubwa kwa mazingira na husababisha jangwa na huku Tanga hali ya ukataji miti kwa ajili ya mkaa iko juu, hivyo tunaamini mpango huu wa kusaidia mitungi ya gesi na majiko hasa wanawake ambao wanaathirika na moshi utakanao na kuni na mkaa utakuwa njia sahihi ya kuondokana na changamoto zilizipo.

Kampuni inawekeza kwa kutekeleza miradi ya kutoa elimu juu ya gesi safi ya kupikia, inachangia vifaa vya gesi ya kupikia katika baadhi ya mikoa.Pia tunahamasisha matumizi ya gesi kwa kufanya mauzo makubwa ya mitungi kwa bei nafuu.

“Juhudi zote hizi zinalenga kufanya Watanzania wengi wanaanza kutumia gesi safi ya kupikia kama alivyoahidi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan ambaye ameweka malengo ifikapo mwaka 2030 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia gesi safi ya kupikia.

“Kampuni ya Oryx Gas Tanzania pia imeitikia mwito wa kidunia ya kupunguza hewa ukaa kutoka viwandani na shughuli za kibinadamu.Hivyo tunayo furaha kuungana na Serikali katika juhudi za kuboresha maisha ya Watanzania kwa kupunguza hewa ukaa,” amesema Benoite.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy Mwalimu pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gas Tanzania Araman Benoite wameshiriki kwenye tukio la ufunguzi wa kituo cha uuzaji na usambazaji wa gesi katika Jiji la Tanga kilichopo Barabara ya Saba , ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha wananchi wanapata kwa urahisi nishati ya gesi pindi wanapoihitaji kwa ajili ya matumizi ya kupikia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Open chat
GREEN WAVES MEDIA
Ahsante kwa kutembeiea UMMY MWALIMU: UMEFIKA WAKATI KWA JAMII KUACHANA NA MATUMIZI YA KUNI NA MKAA