Timu ya Simba SC imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Singida Big Stars ya Mkoani Singida mchezo uliopigwa katika Dimba la Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Wekundu hao wa msimbazi walianza kuhesabu bao la kwanza katika dakika ya 8 ya mchezo huo kipindi cha kwanza,bao hilo likipachikwa kambani na mshambuliaji hatari raia wa Congo Jean Beleke kwa kuunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Clatus Chama.
Simba iliwachukua dakika 12 tu ya kipindi cha kwanza kuhesabu goli la pili ambapo Saidoo Ntibanzokiza alipachika bao hilo akipiga kichwa kuunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Clatus Chama katika dakika ya 20 ya mchezo huo.
Hata hivyo timu ya Singida Big Stars ilipata bao katika dakika ya 43 ya mchezo huo kipindi cha kwanza kupitia mpira wa adhabu uliopigwa na Bruno Gomez na kwenda kambani moja kwa moja na kumshinda mlinda mlango wa Simba Aishi salum Manula.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikilishambulia lango la mwenzake ambapo dakika ya 63 ya kipindi cha pili Pape Osman Sakho aliwanyanyua mashabiki wa msimbazi kwa kupachika bao la tatu kwa ‘tick tack’ akiunganisha Cross ya Shomari Kapombe.
Kufuatia matokeo hayo timu ya Simba inaendelea kushika nafasi ya pili ikiwa alama 56 ikiwa nyuma ya Mabingwa watetezi timu ya Yanga.