Serikali imesema itaendelea kutangaza vivutio vya utalii katika nchi wanazotoka washiriki wa mbio za Kilimanjaro International Marathon ili kuongeza idadi ya washiriki wa mbio hizo na hatimaye kuongeza idadi ya watalii nchini.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii katika mbio za Kilimanjaro International Marathon zilizofanyika mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
“Kupitia Bodi ya Utalii Tanzania tutafanya matamasha ya kutosha ya vivutio vyetu hasa katika nchi ambazo wanatoka washiriki wa mbio za Kilimanjaro International Marathon ili tuongeze idadi ya watalii” Mhe. Masanja amesisitiza.
Aidha, Mhe. Masanja ameahidi kwamba Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana na waandaaji wa mbio hizo ili kuangalia namna bora ya kutumia fursa ya mbio hizo katika kukuza utalii nchini Tanzania na kwamba mbio hizo zinapeperusha bendera ya Tanzania ndani na nje katika sekta ya michezo na utalii.
Amesema Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kutangaza utalii wa Tanzania hivyo ni jukumu la kila mmoja kuendelea kuutangaza utalii kwa nguvu zote.
Amewataka washiriki wa mbio hizo kutumia fursa hiyo kufanya utalii hasa katika Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi na hifadhi nyingine kama Serengeti, Ngorongoro pamoja na Kisiwa cha Zanzibar.
Mbio za Kilimanjaro International Marathon zimekuwa zikifanyika kwa takriban miaka 21 sasa na zimekuwa zikipata washiriki kutoka mataifa mbalimbali duniani na nchini Tanzania.