Home LOCAL WAKURUGENZI MKOA WA SINGIDA WAPEWA DESA LA KUONGEZA MAPATO

WAKURUGENZI MKOA WA SINGIDA WAPEWA DESA LA KUONGEZA MAPATO

OR-TAMISEMI

Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Singida wameshauriwa kufanya makisio sahihi ya mapato ya ndani ya Halmashauri pamoja na kuimarisha ushirikishwaji wa Wakuu wa Idara katika ukusanyaji wa mapato ya ndani hatua itakayopelekea ongezeko la mapato na kuondokana na utegemezi toka Serikali Kuu.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Menejimenti na Ukaguzi Mkoa wa Singida Bw. Evodius Katare Januari 17, 2023 katika kikao cha kufunga taarifa ya tathmini ya vyanzo vya mapato ya ndani ya Halmashauri za Mkoa wa Singida Jijini Dodoma.

Bw. Katare amesema baadhi ya Halmashauri zinakusanya mapato madogo ukilinganisha na hali halisi ya vyanzo vya mapato vilivyopo katika Halmashauri husika na kupelekea upotevu wa mapato ambayo yangetumika katika kuleta maendeleo.

“Inasikitisha sana kuona Idara ndani ya Halmashauri zinakusanya fedha ndogo ukilinganisha na mshahara, posho, motisha, wanazopewa; unakuta Afisa ameajiriwa kwa kazi inayoleta mapato kwa mwaka mzima anakusanya Mil.2 na hii sio Afya kabisa kwa Halmashauri’ amesema Katare

Idara zinazohusika na mapato lazima wawe makini na wajitoe kwa kazi hizi, lazima wafanye kwa moyo kuhakikisha kuwa hakuna upotevu wa mapato na Serikali inapata fedha za mapato inavyotakiwa na sio kuwa wavivu tu na kutokakujali ukusanyani wa fedha za Serikali.

Sambamba na hilo amewashauri Wakurugenzi hao kujifunza na kubadilishana uzoefu kwa Halmashauri zilizofanya vizuri mapato ya ndani,kuibua vyanzo vipya vya mapato pamoja na kuona namna bora ya kuongeza mapato katika Halmashauri husika.

Akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Rais-TAMISEMI ambaye ni Mwenyekiti wa Timu ya Mkoa wa Singida Bi. Nteghenjwa Hosseah amesema kuwa Ofisi ya Rais -TAMISEMI amesema katika zoezi hilo wamegundua kuwa kuna baadhi ya ushuru Halmashauri moja inakusanya wakati nyingine haikusanyi hivyo ni wakati sasa kama Mkoa kuona namna ambavyo Halmashauri zote za Mkoa huo zinakusanya vile vyanzo vinavyofanana bila kuwa na kutofautiana.

Naye Afisa kutoka Idara ya Serikali za Mitaa Ofisi ya Rais-TAMISEMI ambaye pia ni mjumbe wa timu ya Mkoa wa Singida Brian Samuel ametoa rai kwa Halmashauri hizo kuongeza usimamizi wa vyanzo vya mapato,kuweka mikakati thabiti ya kuhakikisha kila chanzo kinakusanya mapato kwa kiwango cha juu pamoja na Halmashauri hizo zijikite katika kilimo cha mazao ya kimkakati.

Zoezi hili limetoa fursa kwa wataalam wa Halmashauri za Mkoa wa Singida kupitia bajeti zao kwa kina, kuongeza wigo wa mapato, kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato na kuandaa bajeti yenye uhalisia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here