Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), imetakiwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii katika utekelezaji wa majukumu yake ili kufikia malengo iliyojiwekea na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wakati kuhusu uhifadhi endelevu wa wanyamapori nchini.
Hayo yamesemwa leo Januari 23,2023 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe. Mary Masanja(Mb) wakati wa kikao kazi na Menejimenti ya TAWIRI kilichofanyika jijini Arusha.
“Mnatakiwa mshirikishe Taasisi zote za Wizara katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali mnayoyafanya kwenye maeneo ya hifadhi hususani doria za kuwarudisha Tembo wanaovamia makazi na mashamba ya wananchi, tafiti za idadi ya Wanyamapori kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na mambo mengine yanayoigusa Taasisi hii “ amesisitiza Mhe. Masanja.
Aidha, ameitaka Taasisi hiyo iendelee kutoa elimu na ufafanuzi juu ya changamoto ya migongano kati ya shughuli za binadamu na Wanyamapori wakali na waharibifu hususan Tembo na kuwaonesha njia salama zinazoweza kutumiwa na wananchi kukabiliana na tatizo hilo, ili kuwe na uelewa wa pamoja kati ya Wataalamu na Waheshimiwa Wabunge.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TAWIRI, Dkt. Eblate Ernest Mjingo akizungumza wakati wa kikao kazi hicho amesema kuwa taasisi hiyo itaendelea kufanya, kuratibu na kusimamia utafiti wa wanyamapori nchini pamoja na kutoa takwimu na ushauri wa kitaalamu ili kuiwezesha Serikali na wadau mbalimbali katika kusimamia uhifadhi endelevu wa wanyamapori hapa nchini.