Home Uncategorized WATUMISHI BRELA WAFUNDISHWA MATUMIZI SAHIHI YA TEHAMA, MAADILI

WATUMISHI BRELA WAFUNDISHWA MATUMIZI SAHIHI YA TEHAMA, MAADILI

Watumishi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), wamejengewa uwezo kuhusu matumizi sahihi ya TEHAMA pamoja na Maadili kwa Watumishi wa Umma, tarehe 3 Desemba, 2022, katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii, jijini Dar es Salaam.

Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, Afisa TEHAMA kutoka BRELA, Bw. Marcel Luboneka amebainisha kuwa kutokana na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kila mtu anapaswa kuwa makini na kila kitu anachokifanya anapotumia mtandao.

Ameeleza kuwa maendeleo katika eneo hilo yameambatana na vihatarishi vingi, mojawapo ikiwa ni kudukuliwa na kuibiwa taarifa mbalimbali ambazo zinapotumika nje ya utaratibu wa kawaida zinaweza kuharibu taswira ya Taasisi na kazi inazozifanya.

Amewataka watumishi hao kuwa makini na utunzaji wa nywila wanazozitumia katika vifaa na mifumo mbalimbali ya Taasisi, kutofautisha vifaa vinavyotumika kubeba nyaraka za ofisi na binafsi, tovuti wanazotembelea pamoja na viunganishi wanavyofungua wakiwa Katika mtandao.

Kwa upande mwingine, watumishi hao wamejengewa uwezo kuhusu sera ya matumizi sahihi ya TEHAMA yanayokubalika. Sera ambayo inatoa mwongozo kuhusu utumiaji wa sahihi wa mitandao na mifumo, ili kuepuka vihatarishi mbalimbali vinavyoweza kujitokeza.

Kwa upande wake Mkurungezi wa Huduma na Uwezeshaji wa BRELA, Bw. Daimon Kisyombe akiwasilisha mada kuhusu Maadili ya Utumishi wa Umma, amesisitiza kuhusu umuhimu wa kujenga utamaduni (Organization Culture) ambao unawezesha Taasisi kufikia malengo yake iliyojiwekea katika Mpango Mkakati wa mwaka 2021/22-2025/26.

Amesema ujenzi wa utamaduni huo ni kazi ya pamoja kati ya viongozi na watumishi wote kwa kuhakikisha kila mtumishi anazingatia Kanuni za Mwenendo na Maadili ya Utumishi wa Umma.

“Watumishi wanapaswa kujiepusha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ikiwemo masuala ya rushwa, ubaguzi wa kila namna, kutoheshimu wateja, kukosa utii, kutozingatia Sheria na Miongozo katika utoaji huduma”, amefafanua Bw. Kisyombe.

Ameongeza kuwa watumishi wote wana wajibu wa kufanya bidii katika kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wa biashara ili kukidhi mahitaji ya wateja, kujenga taswira njema ya Wakala na kufikia malengo ya Mpango Mkakati.

Amesisitiza pia watumishi kujielimisha kuhusu sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayosimamia utoaji wa huduma za Wakala ili kutimiza azma ya kuwa Taasisi inayozingatia na kutoa huduma kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya nchi.

Bw. Kisyombe amesema hatua itakayofuata baada ya mafunzo haya ni kila mtumishi kusoma kwa makini na kusaini Kanuni na Mwenendo wa Maadili ya Utumishi, ili kuonesha dhamira ya kuziishi katika utendaji kazi wa watumishi wa kila siku.

Mafunzo hayo, ni mwendelezo wa utekelezaji wa mpango wa mafunzo mbalimbali kwa Watumishi wa BRELA, ikiwa ni mojawapo ya mkakati wa kuwajengea uwezo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here