Kutoka Dodoma, Desemba 06, 2022.
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel leo Desemba 06, 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Mratibu wa Malaria wa Dunia kutoka Marekani Dkt. David Walton aliyeambatana na wajumbe kutoka CDC, USAID na PMI.
Kikao hicho kimefanyika ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma, kimehudhuriwa na Wataalamu kutoka mpango wa Taifa wa kupambana dhidi ya ugonjwa wa Malaria, kwa pamoja wamekubaliana kushirikiana katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo ili kuutokemeza kabisa ifikapo 2030.
Kwa niaba ya Serikali Dkt. Mollel ameshukuru mpango wa Rais wa Marekani wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria (PMI) kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya Malaria na kufanikiwa kupunguza ugonjwa huo kutoka 15% mwaka 2015 mpaka 7.5% mwaka huu.
Amesema, mikoa ambayo bado inaongoza kwa kiwango kikubwa cha ugonjwa huo ni pamoja na Katavi, Kigoma, Ruvuma, Geita, Mtwara, Lindi na Kagera, huku akitoa wito kwa Wadau kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza afua za mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria ili kuutokemeza.