Na: WAF- DOM
Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu leo Novemba 3, 2022 amepokea mashine 50 zenye uwezo kutibu mabadiliko ya awali Saratani ya shingo ya kizazi kutoka Shirika la Clinton Health Access Initiatives (CHAI) zenye thamani ya Shlingi Milioni 110 kwa ajili ya kusaidia utoaji wa huduma za matibabu katika vituo vya afya nchini.
Katika zoezi hilo lililofanyika katika kituo cha afya Makole Jijini Dodoma, Waziri Ummy ameagiza vituo vya afya vyote kuwa na mashine hizo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi katika maeneo mbalimbali ya nchini na kuweza kunufaika na huduma hizo.
Amesema, Takwimu bado zinaonesha ongezeko la tatizo la Saratani Duniani, huku Wataalamu wakitahadharisha kuwa, endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa vifo vitokanavyo na Saratani vitaongezeka kutoka takribani watu 520,000 mpaka millioni moja kwa mwaka.
Aliendelea kusema kuwa, tatizo la Saratani limekuwa likiongezeka na kukua kila mwaka nchini na kuweka wazi kuwa, takwimu za Kimataifa zinaonesha, inakadiriwa kuwa na takribani wagonjwa wapya wapatao 40,464 kila mwaka na kati hayo 26,945 hupoteza maisha.
Takwimu kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road za mwaka 2021/2022 zinaonesha kwamba Saratani ya mlango wa kizazi ndiyo inayoongoza kuwa na wagonjwa wengi kwa asilimia 36% na saratani ya mlango wa kizazi huchangia asilimia 21% ya vifo vitokanavyo na Saratani.
Aidha, Waziri Ummy amesema, miongoni mwa mikakati ya kupambana dhidi ya Saratani ni pamoja na utoaji wa chanjo yakukinga Kirusi cha HPV kwa wasichana wa umri wa miaka 9 hadi 14, kuongeza vituo vya kutolea huduma za upimaji mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi, na, kutoa huduma ya uchunguzi wa mabadiliko ya awali ya Saratani ya mlango wa kizazi.
Kwa upande mwingine Waziri Ummy amesema, kwa kipindi cha Januari 2021 hadi Juni 2022, jumla ya wanawake 579,768 walifanyiwa uchunguzi wa awali wa mabadiliko ya Saratani ya mlango wa kizazi, huku kati ya hao 23,109 walikutwa na mabadiliko ya awali na kutibiwa.
Mbali na hayo, Waziri Ummy amesema, Wataalam wameweka wazi kuwa, Saratani ya mlango wa kizazi inazuilika inapogundulika mapema, mabadiliko haya ya awali yanaweza kupata tiba papo papo na tatizo kupona kabisa na pasipo kuweza kuingia kwenye hatua ya Saratani.
Mwisho.