Home BUSINESS TFC YAELEZA MIKAKATI YAKE KWENYE WIKI YA HUDUMA ZA KIFEDHA JIJI MWANZA

TFC YAELEZA MIKAKATI YAKE KWENYE WIKI YA HUDUMA ZA KIFEDHA JIJI MWANZA

Afisa habari na Machapisho wa Shirikisho la vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) Naomi Msabaha (kushoto) akizungumza na wageni ambao ni wanafunzi kutoka Chuo cha Uongozi ADEM cha Jijini Mwanza walipotembelea katika Banda la taasisi hiyo kwenye Maonesho ya Wiki ya Huduma za kifedha Jijini Mwanza.

Afisa habari na Machapisho wa Shirikisho la vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) Naomi Msabaha (kushoto) akigawa machapicho mbalimbali kwa wana chuo hao yatakayowawezesha kupata elimu ya ushirika na kufahamu namna taasisi hiyo inavyotekeleza majukumu yake.

Afisa habari na Machapisho wa (TFC) Naomi Msabaha (kushoto) akizungumza na Bi. Mariam Megji (kulia) aliyefika katika Banda la Shirikisho hilo kufahamu kazi wanazozifanya.

(PICHA NA: HUGHES DUGILO)

Na: Hughes Dugilo, MWANZA.

Imeelezwa kuwa wanaushirika nchini wameamua kuanzisha Benki ya Ushirika Tanzania ambapo mchakato huo kwa sasa unaendeshwa na Benki ya ushirika ya kilimanjaro (KCBL) ya mkoani Kilimanjaro.   na upo kwenye hatua nzuri ya kukusanya mtaji,

Hayo yameelezwa na Afisa habari na Machapisho wa Shirikisho la vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) Naomi Msabaha katika mahojiano maalumu yaliyofanyika leo Novemba 23,2022 katika Maonesho ya Wiki ya Huduma za Kifedha yanayoendelea katika viwanja vya Rock City -mall Jijini Mwanza.

Bi. Naomi amesema kuwa ushirika upo kwenye mchakato wa kuwa na Benki yao ya ushirika ambapo jukumu hilo hapo awali lilikuwa linaendeshwa na shirikisho la vyama vya ushirika Tanzania (TFC) lakini kwa sasa jukumu hilo limekabidhiwa kwa Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro (KCBL) na kwamba kazi iliyobaki kwa sasa ni mchakato wa kutafuta mtaji kwaajili ya kuanzisha rasmi  benki hiyo.

“Benki hii ni mkombozi kwa wana ushirika wote hapa nchini pindi itakapoanzishwa ambapo itaweza kuwasaidia wana ushirika wote katika masuala ya mikopo na suala zima la kuweka akiba na maendeleo ya ushirika kwa ujumla” amesema Naomi.

Amesema kuwa zipo faida nyingi za mwanaushirika endapo atajiunga katika Shirikisho hilo kutokana na fursa mbalimbali zinazopatikana kwa mwananchama, ambapo amezielezea fursa hizo kuwa ni pamoja na kutafutiwa masoko na miradi mbalimbali, kutetea vyama vya ushirika katika masuala ya kisheria na kisera kwa ujumla, pamoja na kuibua fursa za uwekezaji katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Akizungumzia ushiriki wao katika Maonesho hayo amesema kuwa lengo hasa ya kushiriki ni kutoa fursa kwa wananchi wa Jiji la Mwanza kujifunza masuala mbalimbali ya ushirika pamoja na kukutana na wadau wa ushirika,  ambapo amesema kuwa wana ushirika wote tayari wameshapata taarifa juu ya uwepo wa taasisi hiyo kwenye maonesho hayo na kwamba kumekuwepo na ongezeko la watu wanaopita kwenye banda lao kupata elimu.

“Tuko kwenye Programu ya kuhamasisha vyama vya kilimo AMCOS kuwa na dirisha la SACCOS kuweza kusaidia wanachama kuweka akiba na kuweza kukopa katika chama cha msingi, ndio maana tunatumia fursa ya maonesho haya kuendelea kutoa uhamasishaji kwa vyama kutumia fursa zilizopo kwenye SACCOS kuweka akiba zao na kukopa” amesema.

Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) kwasasa linatekeleza mpango mkakati wa miaka mitano 2021-2026 katika maeneo manne ambayo ni kuhamasisha na kukuza taswira, muonekano na mtazamo wa ushirika, kuhamasisha ushiriki wa wananchama katika matukio mbalimbali ili kuweza kujitangaza na kujifunza masuala mbalimbali ya kimaendelo, kuongeza uwezo wa kutafuta na kusimamia rasilimali watu, na kuvijengea uwezo vyama vya ushirika katika masuala mbalimbali yakiwemo uongozi na uandishi wa miradi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here