Serikali imesema itaongeza vitendea kazi yakiwemo magari na pikipiki katika Kanda zenye changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu kwa ajili ya kuwezesha kazi ya udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu kunusuru maisha na mali za wananchi wanaoathirika na wanyamapori hao.
Hayo yamesemwa leo Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Maliasili alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Manyoni Magharibi, Mhe. Yahaya Massare aliyetaka kujua mikakati ya Serikali ya kudhibiti Tembo wanaovamia vijiji vya Doroto, Kitaraka, Kamenaga,Gurugu,Muhanga na Njirii.
Ameongeza kuwa Serikali imekuwa ikitekeleza mkakati wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kwa kuimarisha vituo vya Askari wa Wanyamapori nchini ikiwemo kituo cha askari wanyamapori kilichopo katika kijiji cha Doroto Wilayani Manyoni.
“Wizara imeagiza jumla ya magari 35 na pikipiki 50 ambapo Kanda ya Manyoni itapatiwa gari moja na pikipiki mbili ili kuwezesha udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu” Amesema Mhe. Masanja.
Aidha, amefafanua kuwa katika kipindi cha mwaka 2021/22 jumla ya doria 960 zimefanywa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo na kuongeza kuwa Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya mbinu rafiki za kudhibiti wanyamapori hao ambapo Askari Wanyamapori wa Vijiji wa wilaya watapatiwa mafunzo maalum katika Chuo cha Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii – Likuyu Sekamaganga Mkoani Ruvuma.
Mhe. Mary Masanja amesisitiza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kutekeleza mpango wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo mengine yenye changamoto nchini kwa kadri fedha zinavyopatikana.