Home LOCAL WATHIBITI UBORA WA ELIMU YA JUU AFRIKA MASHARIKI WAKUTANA KUWEKA MIKAKATI YA...

WATHIBITI UBORA WA ELIMU YA JUU AFRIKA MASHARIKI WAKUTANA KUWEKA MIKAKATI YA UBORESHAJI WA ELIMU JIJINI DAR

Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Prof. Charles Kihampa akizungumza na wadau walioshiriki mkutano  wa 11 wa Baraza la Uthibiti Ubora wa Elimu ya Juu Afrika Mashariki (EAQAN) unaofanyika kwa siku nne kuanzia leo Septemba 20 hadi 23, 2022 Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mtendaji Baraza la vyuo vikuu Afrika Mashariki Prof. Gaspard Banyankimbona akizungumza alipokuwa akitoa hotuba yake kuelezea majukumu ya Baraza hilo katika Mkutano wa 11 wa Baraza la Uthibiti Ubora wa Elimu ya Juu Afrika Mashariki (EAQAN) Jijini Dar es Salaam.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Profesa William Anangisye akizungumza kwa niaba ya Mgeni rasmi wa Mkutano huo, Waziri wa Elimu Prof. Adolf Mkenda.

Wadau mbalimbali waliohudhuria mkutano huo wakifuatilia hotuba mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na viongozi.

(PICHA ZOTE NA: HUGHES DUGILO)

Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.

Wathibiti Ubora wa Elimu ya Juu Afrika Mashariki wamekutana kwa siku nne Jijini Dar es Salaam kuweka mikakati na kujadiliana namna ya uboreshaji Ubora wa elimu inayotolewa katika Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu katika Ukanada huo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika maojiano maalum wakati wa mkutano huo Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Prof. Charles kihampa amesema kuwa Mkutano huo utafanyika kwa siku nne kuanzia leo Septemba 20 hadi 23, 2022 ambapo amesema kuwa mkutano huo utajadili namna ya ulinganifu wa Elimu ya Juu inayotolewa katika Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu  Afrika Mashariki.

“Mkutano huu unathibishisha kwamba Taasisi za Uthibiti Ubora wa Elimu Afrika Mashariki zinafanyakazi kwa mashirikiano na Taasisi nyingine na Mikutano hii ndio inayojadili ulinganifu wa Elimu ya Juu inayotolewa katika Vyuo vya Afrika Mashariki na hii inasaidia wanafunzi wanaotoka nchi moja kwenda nchi nyingine kutambulika pamoja na wale wanaokweda kufanyakazi”

Amesema kuwa katika ulinganifu wa Elimu wanaojadili kwenye mkutano huo unasaidia kufanya utambuzi wa Vyuo Vikuu vilivyopo ndani ya Afrika Mashariki na kuitambua Shahada iliyotolewa na Chuo husika.

“Katika Mashikiriano haya pia mwanafunzi anaweza kuhama kutoka chuo kimoja kwenda kingine, kwa mfano mtu anaweza kutoka Chuo cha Tanzania anaweza kwenda Chuo chochote cha Afrika Mashariki na kutoka chuo kingine ndani ya Afrika Mashariki akahamia Chuo chochote cha hapa Tanzania ndio faida ya haya mashirikiano” amesema Prof. Kihampa.

Aidha amesema kuwa yapo mashirikiano ya Ulinganifu wa Elimu ya Juu nje ya Afrika Mashariki kupitia Baraza la Uthibiti la Elimu ya Juu la Afrika Mashariki (EAQAN) unaosaidia kuwepo na mashirikiano ya Taasisi za Elimu ya Juu kati ya Afrika Mashariki na Mataifa mengine ndani ya Afrika na Dunia kwa ujumla.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Profesa William Anangisye akizungumza kwa niaba ya Mgeni rasmi wa Mkutano huo, Waziri wa Elimu Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa uwepo kwa usimamizi madhubuti wa ubora wa Elimu inayotolewa kwenye Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki utawezesha kuwepo kwa wahitimu wenye uwezo watakaokidhi viwango vya Kimataifa na Kikanda.

Amesema kuwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha vyuo na Taasisi za Elimu ya Juu hapa nchini vinatoaa elimu yenye ubora wa Kimataifa na wahitimu wake wamekuwa wakifanya vizuri katia soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Aidha amesisitiza kuwa vyuo vya Afirka mashariki vishirikiane kuhakikisha kwamba ubora unapatikana kwa kuzalisha wahitimu wenye ubora na uwezo wa kimataifa na kikanda.

“Sisi tunasisitiza vyuo vikuu lazima vitoe wahitimu wenye ubora hatutaendelea kusisitiza suala la viwango,  Vyuo lazima vifundishe kwa kufuata viwango ambavyo vitasababisha kuzalisha wahitimu ambao watashindana kwenye viwango vya kimataifa” amesisitiza Prof. Andangisye.

Ameongeza kuwa Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki vinapaswa kuhakikisha wanatumia njia wezeshi kwa wanafunzi kuendelea na masomo panapotokea majanga yatakayosababisha Vyuo kufungwa na kwamba mafunzo yanaweza kuendelea kwa njia ya mtandao (E-Leaning) yatakayowawezesha wanafunzi kujisomea wakiwa nyumbani.

“kipindi cha mlipuko kama ule wa ugonjwa wa korona, Taasisi nyingi katika Afrika Mashariki zilifungwa kwaajili ya kukabiliana na janga hilo. Lakini ikaonekana njia rahisi ya kutatua tatizo hilo ni kutilia mkazo kujifunza katika mtandao ili majanga yanapokuja suala la kusomesha wanafunzi liweze kuendelea” ameongeza.

Katibu Mtendaji Baraza la vyuo vikuu Afrika Mashariki (EAQAN) Prof. Gaspard Banyankimbona amesema kuwa huu ni mwaka wa 11 kufanya Mkutano huo na kwamba kila mwaka mkutano huo unafanyika katika nchi moja kwa kupokezana.

Amesema kuwa ili nchi za Afrika Mashariki ziweze kuwa na kiwango cha Elimu ya ushindani wa Dunia lazima kuwepo na ulinganifu wa Elimu ambapo katika ulinganifu huo wanahakikisha Mamlaka za Uthibiti Ubora zinafanyakazi kwa kushirikiana ili nchi zote kuwepo na uwezo sawa wa ufundishaji.

Ameongeza kuwa kufanya hivyo kutawezesha wahitimu wa Elimu ya Juu kwenda katika nchi yoyote Duniani na kuingia kwenye ushindani wa soko la ajira kutokana na ulinganifu wa Ubora wa elimu aliyoipata kutoka katika nchi yake.(PICHA MBALIMBALI ZA WASHIRIKI WA MKUTANO HUO)

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here