Kutoka New York, Marekani.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa ushirikiano na serikali miradi ya kimataifa wa Taasisi ya The Susan Thompson Buffet Foundation Dkt. Tewodros Bekele Endailalu ili kuongeza miradi ya ushirikiano baina ya nchi hizo katika kuboresha Sekta ya Afya nchini.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika kikao Cha Pembezoni wakati wa Mkutano Mkuu wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) unaoendelea jijini New York nchini Marekani.
Katika kikao hicho, Waziri Ummy aliishukuru Taasisi ya Sussan Thompsom Buffet Foundation Kwa kuisaidia Tanzania katika mradi wa kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto pamoja na utayari wa kuimarisha mifumo ya afya ya jamii hususan wahudumu wa afya vijijini.
Aidha, Waziri Ummy aliiomba taasisi hiyo kuendelea kuisaidia Tanzania katika kuimarisha huduma za udhibiti wa magonjwa yasiyoambukiza na utekelezaji wa mkakati wa Bima ya afya Kwa wote unaotarajiwa kuanza hivi karibuni nchini.
Sambamba na hilo, Waziri Ummy amemualika Dkt. Tewodros kutembelea Tanzania na kuona maendeleo ya utekelezaji wa mradi, na namna inavyosaidia kuboresha huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake Dkt. Tewodros alimhakikishia Waziri Ummy kuwa, Taasisi ya Sussan Thompsom Buffet Foundation Iko tayari kuisaidia Tanzania kulingana na vipaumbele vya nchi vinavyolenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Mwisho.