Na Dotto Mwaibale, Singida.
SERIKALI imefanya marekebisho ya Sheria ya Mahakama za Utatuzi wa migogoro
ya ardhi namba 216, ambapo mabaraza ya
kata yameondolewa uwezo wa kusikiliza mashauri ya ardhi kama yalivyo kuwa
yakifanya awali.
Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Wilaya ya Singida, Bahati Colex, alisema hayo
leo wakati wa semina ya wenyeviti wa mabaraza ya kata wa Manispaa ya Singida
kuhusu mabadiliko ya sheria ya mahakama za utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Alisema marekebisho hayo ya sheria yanalenga kuboresha utoaji haki hasa
ukizingatia kuwa jukumu hili yalipewa mabaraza ya kata ambayo kimsingi wajumbe
wake si wataalamu wa sheria, hali iliyosababishwa kufutwa kwa maamuzi yao mengi
kutokana na makosa ya kisheria kama kutotimia kwa akidi.
Colex alisema kufuatia marekebisho hayo ya sheria ambayo yalianza kutumika
rasmi 11 Oct,2021mabaraza hayo ya kata yamepewa jukumu la usuluhishi tu ambao utatakiwa kufikiwa ndani ya siku 30
kutoka siku shauri lilipofunguliwa.
Alisema usuluhishi ukishindikana mabaraza ya kata yatatoa cheti cha
usuluhishi ili wadaawa waweze kufungua shauri lao kwenye baraza la ardhi na
nyumba wilaya na kwamba hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 13(2),13(4) vya Sheria
ya mahakama za utatuzi wa migogoro ya ardhi kama ilivyorekebishwa na Kifungu
cha 45 cha Sheria no.5/2021 “The Written Laws (miscellaneous Amendments) (No.3)
Act, 2021.
“Kifungu cha 45 cha sheria hii kimerekebisha kifungu cha 13 (2) na
kuyapa mabaraza ya kata jukumu la usuluhishi tu badala ya kusikiliza kesi na
kutoa hukumu, sasa mabaraza ya kata yanapaswa kusuluhisha mgogoro wa ardhi kati
ya wadaawa ndani ya siku 30 kwa mujibu wa Kifungu cha 13 (4),”alisema.
Colex alisema kwa mujibu wa mabadiliko hayo ya sheria mashauri yote ya
ardhi yataanzia kwenye mabaraza ya kata bila kujali thamani ya ardhi husika,
Kifungu cha 13 (4) kinaeleza kuwa mabaraza ya ardhi na nyumba wilaya
halitasikiliza shauri lolote la ardhi mpaka baraza la kata lithibitishe kuwa
limeshindwa kusuluhisha.
Alisema Baraza la Kata likishindwa kuwasuluhisha wadaawa litatoa cheti au
hati ya usuluhishi ambapo wadaawa
watakuwa na nafasi ya kufungua shauri lao la ardhi katika baraza la ardhi na
nyumba wilaya.
Aidha, ikiwa siku 30 zitapita toka lalamiko lilipopelekwa baraza la kata
bila kusuluhishwa, mlalamikaji anaruhusiwa kufungua shauri lake mbele ya baraza
la ardhi na nyumba wilaya bila hata kuwa na cheti cha usuluhishi.
Aliongeza kuwa sheria hiyo pia inampa mamlaka Waziri wa Sheria
akishirikiana na Waziri wa Ardhi kutengeneza kanuni zitakazo simamia uendeshaji
wa usuluhishi mbele ya mabaraza ya kata, Kifungu cha 13 (5) kama kilivyofanyiwa
marekebisho na Kifungu cha 45.
“Sheria hii kupitia Kifungu cha
46 na 47 imefuta Kifungu cha 15 ambacho ni sawa na Kifungu cha 10 cha Sheria ya
Mabaraza ya kata ambavyo vinahusu uwezo wa mabaraza ya kata kusikiliza mashauri
ya ardhi yasiyo zidi thamani ya milioni tatu, Imefuta Kifungu cha 16 ambacho
kinahusu mamlaka ya mabaraza ya kata yanaposikiliza mashauri ya ardhi, Imefuta
Kifungu cha 20 kinachohusu rufaa na muda wa kukata rufaa, na imefuta Kifungu
cha 21 kilichokuwa kinampa nguvu waziri kutengeneza kanuni za kuendesha rufaa
kutoka baraza la kata kwenda baraza la ardhi na nyumba wilaya,” alisema.
Colex alisema kuhusu mashauri ya
ardhi yaliyofunguliwa kabla ya 11 Oct,2021 mbele ya Mabaraza yakata a kabla ya
mabadiliko haya ya sheria yataendelea kwa utaratibu wa zamani na yatatolewa
hukumu.
“Kwakuwa mabadiliko haya ya sheria yalianza 11 Oct, 2021, mashauri
yote yaliyofunguliwa baada ya mabadiliko haya ambayo yanasikilizwa badala ya
kusuluhishwa yanasikilizwa kimakosa mbele ya mabaraza hayo ya kata kwakua hayana mamlaka ya
kusikiliza na kutoa hukumu hivyo mashauri hayo yanapaswa kusuluhishwa tu, na
kwa yaliyotolewa hukumu basi hukumu hizo zitakuwa batili kwenye macho ya sheria
kwakua zinatokana na mabaraza yasiyo na mamlaka kisheria,” alisema.
Mwanasheria wa Manispaa ya Singida, Burton Mahenge, alisema wajumbe wa
Baraza la Kata wanapomaliza muda wao wa miaka mitatu wawe wanatoa taarifa
mapema ili kutoa fursa kufanyika mchakato wa kupata wajumbe wapya.
Mahenge alisema wajumbe wanapochelewa kutoa tangazo la kumaliza muda wao
kunasababisha uchelewaji wa usikilizwaji wa mashauri.
Nao wenyeviti wa kata Manispaa ya Singida walilishukru Baraza la Ardhi
Wilaya ya Singida kwa kuitisha semina hiyo ambapo walisema mambo waliyofundishwa
yatawajengea uelewa zaidi hasa baada ya serikali kufanya mabadiliko ya Sheria za mahakama za utatuzi wa migogoro ya Ardhi.
Walisema mafunzo hayo yatawawesesha kufanya kazi kwa ufanisi na kuacha
kufanya kwa mazoea hali itakayowezesha upatikanaji wa haki kwa wakati.
Aidha,
waliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwaongezea posho ya kukaa kwenye
vikao vya Baraza la Kata ambapo walisema kiwango cha Sh.1000 kinachotolewa kwa
kikao kimoja hakitoshelezi kabisa kwakuwa baadhi yao wamekuwa wakitoka maeneo
ya mbali. na kuwa kimepitwa na wakati.