Pikipiki nane zilizokabidhiwa kwa mameneja wa RUWASA mkoa wa Geita |
Na: Costantine James, Geita.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe, Martin Shigella amezitaka jumuiya za watoa huduma ya maji ngazi ya Jamii ( CBWSO’s) Mkoa wa Geita Kuzingatia bei elekezi ya uuzaji wa maji kwa wananchi kama ilivyoelekezwa na wizara ya maji hapa nchini.
Mhe,Shigella amebainisha hayo wakati akikabidhi pikipiki nane kwa mameneja wa Mamlaka ya maji na usafi wa mazigira vijijini (RUWASA) mkoa wa Geita katika ofisi za RUASA mkoa wa Geita.
Amezitaka jumuiya za watoa huduma ya maji Mkoani humo (CBWSO’s) kuheshimu kanuni na taratibu zilizotolewa na Serikali kupitia wiazara ya maji chini ya waziri Juma Aweso kufata bei ya maji zilizoanza kutumika Agosti 1, 2022.
Shigella amesema Serikali imetoa muongozo wa bei elekezi za maji katika jumuiya za watoa huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSO’s) kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata huduma ya maji safi na salama kwa bei nafuu zaidi ili waondokane na kero ya ukosefu wa maji safi na salama.
Mhe, Shigella amesema Wizara ya Maji imetoa bei elekezi ambapo kwa upande chanzo cha maji kinachotumia mashine inayotumi dizeli, ndoo moja haipaswi kuzidi Sh50, kwa msukumo wa nguvu ya umeme ni sh 40 na maji yanayopatikana kwa umeme wa jua ni sh 30 na maji ya mserereko ndoo isizidi Sh 25.
Amewataka wale wote waliokabidhiwa pikipiki hizo kuachana na tabia ya kuvutumia kwa malengo binafsi kwa kuwapa vijana kuzitumia kwenye biashara ya bodaboda ili kujiingizia kipato kinyume na malengo yaliyokusudiwa.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Geita Mhandisi Jabir Kayilla wakati akisoma taarifa mbele ya mkuu wa Mkoa Martin Shigella amesema mahitaji ya maji vijijini ndani ya mkoa wa Geita ni lita milioni 53.4 lakini kwa sasa yanayozalishwa ni lita milioni 36.3 hivyo kuwa na upungufu wa lita 17.1 milioni sawa na asilimia 32%.
Amesema RUWASA mkoa wa Geita inatekeleza ya maji miradi 16 pamoja na uchimbaji wa visima 36 katika maeno mbalimbali ya mkoa huo na miradi hiyo ikikamilika itaongeza hali ya upatikanaji wa maji kutoka asilimia 68% zilizopo kwa sasa hadi kufikia asilimia 76%.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA wilaya ya Geita Mhandissi Sande Batakanwa ameipongeza serikali kwa kuwapa vitendea kazi hivyo kwani vitaenda kuwasaidia katika utekelezaji wa miradi ya maji Vijijini.