Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Dkt. Francis Michael ameyafunga rasmi Maonesho ya 17 ya Eimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) yaliyokuwa yakifanyika kwa siku sita katika viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu huyo amesema kuwa Wizara kupitia TCU itaendelea kutoa mafunzo ya kubadilishana uzoefu ya kitaaluma na mbinu bora za ukusanyaji wa maoni ya wadau na vigezo vya uandaaji na uhuishaji wa mitaala itakayozingatia mahitaji ya wadau na soko la ajira.
Dkt. Michael ameyasema hayo leo Julai 23,2022 katika hafla ya kuyafunga rasmi Maonesho ambapo Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu vilipata fursa ya kukutana na wananchi mbalimbali na kufanya udahili wa papo kwa hapo.
Aidha amesema kuwa Serikali inaendelea na programu mbalimbali za maboresho ya elimu katika Taasisi za Elimu ya Juu ambapo katika mwaka huu wa fedha zaidi ya mitaala 300 inafanyiwa mapitio na kuhuishwa kwa kuzingatia maoni ya wadau ili kukidhi matarajio yao.
“Wizara imesaini Dola za kimarekani milioni 625 kwa ajili ya kujenga Vyuo Vikuu Vishiriki katika Mikoa ambayo isiyokuwa na vyuo vikuu, na Tanzania Bara na Zanzibar kote watapata vyuo vikuu vishiriki ambavyo baadae vitatanuka na kuwa vyuo vikuu,” Amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TCU Prof. Penina Muhando amesema kuwa lengo la kufanyika kwa Maonesho hayo ni pamoja na kuimarisha mahusiano baina ya taasisi hizo na kutoa fursa kwa Taasisi hizo kuweza kukutana na wanafunzi wanaotaka kufanya udahili wa kujiunga na Masomo.
“Maonesho haya yatawezesha wananchi kupata fursa za kuona shughuli mbalimbali zinazotendwa na taasisi za elimu ili kuwasaidia wanaotaka kuendelea na elimu ya juu kufanya maamuzi ya kujiendeleza”. Amesema Prof.Muhando.
Maonesho ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yalifunguliwa rasmi Julai 18 mwaka huu na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ambapo leo Julai 23,2022 yamefikia tamati.