Home BUSINESS “SULUHISHA NA BRELA” YAWAKOSHA WAWEKEZAJI

“SULUHISHA NA BRELA” YAWAKOSHA WAWEKEZAJI


Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imepongezwa kwa kuja na wiki ya Suluhisha na BRELA, yenye lengo la kutatua migogoro mbalimbali katika kampuni.

Akizungumza baada ya kupata huduma katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa uliopo mtaa wa Shaaban Robert, mkabala na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM),  leo tarehe 16 Juni, 2022, Jijini Dar es salaam,
 Bw .Theophil Kimaro ambaye ni Mkurugenzi  wa kampuni ya TRINE CONSULT, amesema huduma hii imetoa mwaga  kwake na amepata suluhu ya changamoto iliyokuwa ikimkabili.

Ameongeza kuwa kabla ya kufika BRELA alishindwa kuipatia ufumbuzi wa haraka changamoto iliyokuwa inamkabili, lakini baada ya kufika na kuzungumza na maafisa wa BRELA suala lake limepatiwa ufumbuzi wa haraka na amepewa ushauri wa kujenga  hivyo ataondokana na migogoro katika kampuni yake.

“Haikuwa rahisi kuepukana na lililokuwa likinitatiza lakini baada ya kupata matangazo kuwa kuna Suluhisha na BRELA,  nimelazimika kufika ili kupata huduma na hakika haijachukua hata zaidi ya nusu saa, tayari suala langu wamelimaliza na sasa naenda kulifanyia kazi,” amefafanua Bw.  Kimaro.

Bw. Kimaro ameitaka  BRELA kufanya kampeni kama hii mara kwa mara ili  wadau wengi wapate fursa ya kushauriwa na kutatuliwa changamoto zao.

Kampeni Maalum ya “Suluhisha na BRELA” iliyoanza tarehe 13 Juni, 2022 itahitimishwa tarehe 19 juni, 2022.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here