Home BUSINESS SERIKALI KUAJIRI ASKARI 600 KUKABILIANA NA WANYAMA WAKALI NA WAHARIBIFU

SERIKALI KUAJIRI ASKARI 600 KUKABILIANA NA WANYAMA WAKALI NA WAHARIBIFU

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akijibu swali Bungeni jijini Dodoma leo Juni 1,2022.

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeomba kibali cha kuajiri askari wa uhifadhi wapya 600 ambao watasambazwa kwenye maeneo hatarishi ili kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu. 

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum, Mhe. Jacqeline Ngonyani Msongozi,  aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuwadhibiti tembo wanaovamia, kuharibu mazao na kujeruhi wananchi katika kata za Mindu, Kalulu na Tinginya, Wilaya ya Tunduru.

Mhe. Masanja ameongeza kuwa Wizara ina mkakati wa kuanzisha vituo vya kikanda vya Askari katika maeneo yenye changamoto ya  wanyamapori wakali na waharibifu.

Pia, amesema Serikali itatoa mafunzo kwa askari wa wanyamapori wa vijiji; na kuelimisha wananchi kuhusu namna bora ya kupunguza athari zinazotokana na wanyamapori wakali na waharibifu.

Katika hatua nyingine, akijibu swali kuhusu mikakati ya Serikali ya kutangaza maporomoko ya Kalambo Mhe. Masanja amefafanua kuwa Wizara itatumia vyombo vya habari, itaandaa machapisho na majarida na kushiriki katika maonesho, matamasha, matukio na makongamano ya utalii na biashara yanayofanyika ndani na nje ya nchi ili kutangaza kivutio hicho.

Pia amesema njia ya kuweka mabango katika viwanja vya ndege ikiwemo uwanja vya ndege wa Songwe na maeneo mengine katika Mkoa wa Rukwa itatumika kutangaza utalii huo. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here