Home LOCAL NASSARI SASA AELEWA UMUHIMU WA DC KUPEWA MAMLAKA YA KUWEKA MTU KIZUIZINI...

NASSARI SASA AELEWA UMUHIMU WA DC KUPEWA MAMLAKA YA KUWEKA MTU KIZUIZINI SAA 48

MARA.

MKUU wa Wilaya ya Bunda katika Mkoa wa Mara, Joshua Nassari ambaye amewahi kuwa Mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Tanzania, kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ameeleza umuhimu wa wakuu wa wilaya kuwa na mamlaka kisheria, kumweka Mtu rumande kwa Saa 48.

Wakati huo huo amekiri kwamba alipokuwa bungeni alikuwa miongoni mwa wabunge vinara waliopinga uwepo wa sheria hiyo, wakiamini ilitumiwa vibaya dhidi ya wananchi, wakiwemo watumishi wa umma katika kada tofauti.

Sasa akiwa DC anaelezea jinsi mamlaka hayo yanavyomuwezesha kudhibiti watu wasiyokubali kutekeleza wajibu wao kwa misingi ya taratibu, miongozo, kanuni na sheria  zilizowekwa kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali nchini.

Nassari alisema hayo baada ya kulazimika kuingilia kati mvutano uliyotokea kati ya Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) wa Wilaya ya Bunda, Mhandisi Baraka Mkuya na Mkurugenzi wa Kampuni ya CYM inayojenga moja ya barabara za Mfuko wa Jimbo, Magige Wambura ndiyo uliyomuibua DC Nassari.

Walikuwa kwenye kikao cha viongozi wa kisiasa na kiserikali mkoani Mara, wakuu wa wilaya, mameneja wa mkoa na wilaya wa taasisi zinazosimamia utekelezaji wa miradi ya maji, barabara na umeme kilichofanyika chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi.

“Kwa bahati mbaya au nzuri nilikuwa mwanasiasa wa upinzani, Mmoja wa wabunge waliopinga mkuu wa wilaya kuwa na mamlaka ya kuweka Mtu rumande kwa muda usiyozidi Saa 48 lakini sasa nimeelewa umuhimu wake,” alisema Nassari.

Alisema licha ya Wambura kuwa na umri unaorandana na baba yake mzazi, amejikuta akishindwa kujizuia kutumia mamlaka hayo dhidi yake na kwamba ameisha muweka rumande mara Mbili kwasababu anawatesa sana wanapotimiza wajibu wao wa kusimamia  utekelezaji wa mradi unaotekelezwa naye.

Katika kikao hicho kila meneja wa mkoa alitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi iliyo chini ya taasisi anayosimamia akifuatiwa na taarifa ya meneja wa wilaya, huku wakandarasi ‘vimeo’ wakitakiwa kujieleza ili malengo washiriki wa kikao wapete uelewa wa pamoja na inapowezekana ufumbuzi wa changamoto upatikane.

Ni katika utaratibu huo ambapo Meneja wa TARURA-Mkoa, Mhandisi Boniface William alipotaja Halmashauri ya Bunda kuwa kinara wa kukwamisha utekelezaji wa miradi.

Naye Mhandisi Mkuya katika taarifa yake ya wilaya alitaja wakandarasi Wanne eanaosababisha mdororo huo, akiwemo CYM ambaye kwa mujibu wa utaratibu wa kikao hicho alitakiwa kujieleza.

Mkandarasi mwingine  aliyetajwa kuwa ni kimeo zaidi ni NODICA ambaye Mkuya alisema walimzuia kuhudhuria kikao hicho kwa kuhofia angewatoroka, kwamba baada ya kutoonekana site kwa muda mrefu alisakwa kwa kutumia polisi mpaka akapatikama na kwa wakati huo alikuwa saiti huku akilindwa na polisi.

‘Huyo amezuiwa kutoka nje ya Bunda mpaka atakapokabidhi mradi,” anasema Mhandisi Mkuya.

Ilibainika kuwa Mhandisi huyo (NODICA) ana mikataba ya kutekeleza miradi katika wilaya nyingine mbili, ikiwamo Rorya ambapo wakuu wa wilaya hizo kwa nyakati tofauti walikieleza kikao kuwa hata wao walishaelekeza polisi wamtafute Mkandarasi huyo.

Kwa upande wa Wambura, katika hali iliyoashiria hakuwa akieleza ukweli, alishauriwa na Mhandisi Mkuya kwamba aeleze ukweli ili kikao kimsaidie kwani alitakiwa kukamilisha mradi tangu Machi Mwaka huu, hajaukamilisha na alipotea saiti kwa takriban miezi miwili.

Katika hali iliyoashiria kutofurahishwa na ushauri huo, alisema;

“Haya sasa, sikuwa saiti kutokana na meneja kukataa kuidhinisha hatua moja ya kazi yangu ili niendelee na nyingine, kwasababu ambazo sikukubaliana nazo na baadaye meneja huyo huyo akaniambia, “sasa unawe kuendelea.” na niliandika certificate lakini mpaka sasa sijalipwa.”

Mnyukano huo wa hoja ulizimwa na DC Nassari akisema; “Huyu mzee ana umri sawa na Baba yangu lakini nimeishamuweka rumande mara Mbili na kumtoa baada ya muda mfupi, anatusumbua sana huyu mzee.”

Moja ya matendo ya kukera waliyowahi kutendewa na Mkandarasi huyo lilielezwa na DC Nassari kuwa ni kuharibu miundombinu ya maji hali iliyowakosesha watu huduma hiyo na hata baada ya TARURA, BUWASA na DC kwa nyakati tofauti kumtaka alipe Sh 70,000 kugharamia  matengenezo ya miundombinu hiyo, alikataa na kutoonekana saiti mpaka aliposakwa kwa polisi.

Kupitia vikao kazi kati ya mkandarasi huyo, Tarura na DC, alidai aliishiwa fedha ndiyo maana hakuwa saiti, akashauriwa kuandika madai ili alipwe, akafanya hivyo yapata wiki tatu zilizopita, maelezo ambayo yalitowa nguvu  na Mhandisi William, kwamba certificate hiyo inashughulikiwa ofisini kwake.

RC Hapi alisema katika kikao hicho kuwa imethibitika wakandarasi wazawa ambao walilalamika kunyimwa kazi, sasa wanapewa kazi na kuzichezea jambo ambalo halitaendel3a kuvumiliwa.

Previous articleTIGO YAJA NA SULUHISHO ULIPAJI WA MAEGESHO MLIMANI CITY
Next articleMKUU WA MKOA WA RUVUMA AKABIDHI PIKIPIKI 286 KWA MAAFISA UGANI,AWATAKA KWENDA KUSIMAMIA NA KUONGEZA UZALISHAJI WA MAZAO MASHAMBANI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here